×

Rais Samia Azindua Mpango Elekezi wa Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika

Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akizungumza kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026) Jijini Addis Ababa nchini Ethiopia. Mkutano huo mkubwa wa kimataifa unawakutanisha viongozi wa Serikali, mawaziri wa afya, wataalamu wa afya, wanasayansi, watafiti na washiriki wa maendeleo kutoka Afrika na duniani.

ADDIS ABABA, ETHIOPIA – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika, unaolenga kupunguza vifo vya uzazi na watoto wachanga pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

Uzinduzi huo umefanyika leo, Novemba 23, 2026, jijini Addis Ababa, Ethiopia, wakati wa Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026).

Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa pamoja na viongozi mbalimbali kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), Jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 23 Novemba, 2026.

Rais Dkt. Samia, ambaye pia ni Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, amezitaka nchi za Afrika kuharakisha hatua za kukomesha vifo vya uzazi na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Samia amesema kulinda akina mama, kuwalinda watoto na kuwawezesha vijana ni majukumu ya msingi ya uongozi, akisisitiza kuwa hatua hizo zinahitaji ufadhili endelevu na uwajibikaji thabiti.

Ameeleza kuwa mwaka 2023, wanawake takribani 180,000 walifariki kutokana na sababu za uzazi barani Afrika, huku watoto wachanga milioni 1.18 wakipoteza maisha.

Rais Samia, akiwa na Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, kwenye picha na viongozi mbalimbali wanaoshiriki kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), Addis Ababa, Ethiopia.

Akizungumzia hali ya Tanzania, Rais Dkt. Samia amesema takwimu mpya zinaonesha kuwa vifo vya uzazi nchini vimeshuka hadi takribani 75 kutoka vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000.

Amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Gates Foundation katika kupunguza vifo hivyo nchini. Ameongeza kuwa uzinduzi wa matokeo ya utafiti huo utafanyika Novemba 26, 2026, jijini Dar es Salaam.

Mpango Elekezi huo unaweka malengo ya Sifuri Tatu kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, ikiwemo kuhakikisha hakuna mjamzito anayefunguliwa katika kituo cha afya bila kuhudumiwa na mtaalamu.

Rais Samia akisalimiana na Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia.

Malengo mengine ni kukomesha vifo vya uzazi na vya watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika, pamoja na kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo.

Ili kufanikisha utekelezaji wa mpango huo, Rais Dkt. Samia amezitaka nchi wanachama kuteua waratibu wenye mamlaka na kuingiza malengo ya Mpango Elekezi katika utekelezaji wa mikakati yao ya kitaifa ya afya.

Rais Samia akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (CDC) Dkt. Jean Kaseya baada ya kuwasili katika Kituo cha Mikutano cha African International Convention Centre (AICC), Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya kushiriki kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), tarehe 23 Novemba, 2026.

Katika kuimarisha watoa huduma wa sekta ya afya, Rais Samia ametangaza ufadhili wa awali wa nafasi 60 za mafunzo ya ubobezi kwa nchi za Afrika.

Mafunzo hayo yatahusu ukunga, usingizi na ganzi, uzazi na magonjwa ya wanawake, pamoja na huduma kwa watoto wachanga, sambamba na mafunzo mafupi ya vitendo chini ya usimamizi wa wataalamu wa tiba wa ngazi ya kati, wauguzi na wakunga.

Mkutano wa CPHIA 2026 umehudhuriwa na washiriki mbalimbali, wakiwemo wakuu wa nchi na Serikali za Afrika, Rais wa Burundi na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika,  Évariste Ndayishimiye; Rais wa Sierra Leone,Julius Maada Bio; na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dkt. Abiy Ahmed Ali.

Wengine ni Makamu wa Rais wa Uganda,  Jessica Alupo, na Waziri Mkuu wa Rwanda, Dkt. Justin Nsengiyumva.

Rais Samia akizungumza na Evariste Ndayishimiye, Rais wa Jamhuri ya Burundi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), baada ya kuwasili katika Kituo cha Mikutano cha African International Convention Centre (AICC), Addis Ababa, Ethiopia.

Mkutano huo unaendelea jijini Addis Ababa, ukijadili hatua za kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje na kuongeza ufadhili wa ndani na uzalishaji wa dawa na chanjo barani Afrika.

Aidha, Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto kwa kushirikiana na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), inatarajia kuendesha mazungumzo ya ngazi ya juu Novemba 24, 2026, jijini Addis Ababa, kuhusu utekelezaji wa mpango uliozinduliwa.

Rais Samia akiwa kwenye mazungumzo na Julius Maada Bio, Rais wa Sierra Leone.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Dkt. Abiy Ahmed Ali, pamoja na Waziri wa Nchi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Mhe. Sheikh Shakhboot bin Nahyan Al Nahyan, pembeni mwa mkutano wa CPHIA 2026.

Leave a Comment