Rais wa Marekani, Donald Trump akiongea jambo Rais wa Urusi, Vladimir Putin walipokutana China.Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema amemtaka Rais wa Urusi, Vladimir Putin, kusitisha vitendo vyote vya uchokozi wa kijeshi dhidi ya maeneo mbalimbali ya Ulaya, hatua inayokuja wakati juhudi za kutafuta suluhu ya vita kati ya Urusi na Ukraine zikiendelea.
Trump alitoa kauli hiyo kupitia mtandao wake wa Truth Social siku ya Alhamisi, akifafanua kuwa alizungumza na Putin kuhusu suala hilo walipokutana nchini China wiki iliyopita.
Alisema ombi lake kwa kiongozi huyo wa Urusi lililenga kufungua njia ya kufikiwa kwa makubaliano ya kumaliza vita vinavyoendelea nchini Ukraine.
Katika ujumbe wake, Trump alisema anaamini kuna uwezekano mkubwa wa kufikiwa kwa makubaliano kati ya Moscow na Kyiv kwa haraka ikiwa pande husika zitachukua hatua zinazofaa.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Trump kukutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Mark Rutte, katika jimbo la Florida, Marekani. Katika taarifa yao ya pamoja, viongozi hao walisisitiza umuhimu wa Urusi kuepuka hatua zinazoweza kupanua vita vya Ukraine.
Hata hivyo, Trump hakufafanua maeneo mahsusi ya Ulaya aliyoyarejelea katika wito wake huo, wala hakulitaja moja kwa moja Ukraine katika ujumbe wake.
Nchi za Ulaya zimeendelea kueleza wasiwasi kuhusu kile wanachokiona kuwa vitendo vya uchokozi kutoka Urusi. Wasiwasi huo umeongezeka kufuatia taarifa za makombora matatu ya Urusi kuanguka nchini Poland, mwanachama wa NATO, wiki iliyopita.
Trump Abadili Lugha Kuhusu Putin
Kauli ya hivi karibuni ya Trump imekuja ikiwa na tofauti na msimamo wake wa wiki iliyopita alipokutana na Putin katika mji wa Shenzhen nchini China, ambako alimwelezea kiongozi huyo wa Urusi kama rafiki yake.
Hali hiyo ilikuwa imeibua wasiwasi kwa Ukraine na baadhi ya mataifa ya Ulaya kuhusu mwelekeo wa Marekani katika kushughulikia vita hivyo.
Alipoulizwa kama amekuwa mkali zaidi dhidi ya Putin, Trump alisema hana uhakika kama msimamo wake umebadilika, huku akikumbusha kuwa wakati wa muhula wake wa kwanza aliidhinisha mauzo ya makombora ya Javelin kwa Ukraine.
Aidha, Trump alisema hajui kama Putin atahudhuria mkutano wa viongozi wa G20 utakaofanyika Miami mwezi ujao, lakini alieleza kuwa kiongozi huyo wa Urusi ataruhusiwa kuhudhuria iwapo atapenda kufanya hivyo.
Mazungumzo ya Amani Yakabiliwa na Changamoto ya Ardhi
Wakati huo huo, Jared Kushner, mkwe wa Trump ambaye anashiriki katika juhudi za kidiplomasia kuhusu vita vya Ukraine pamoja na Steve Witkoff, ameeleza kuwa suala la maeneo ya mashariki mwa Ukraine yanayodaiwa na Urusi bado ni kikwazo kikubwa katika mazungumzo ya amani.
Katika mahojiano na MD Meets Podcast ya Ujerumani, Kushner alisema suala la mipaka na maeneo yanayodaiwa na Moscow bado halijapata mwafaka.
Pia alionya kuwa makosa ya kimahesabu au hatua zisizotarajiwa zinaweza kusababisha vita hivyo kuongezeka kwa kiwango kikubwa.
Kwa sasa, macho ya mataifa ya Ulaya na jumuiya ya kimataifa yanaendelea kuelekezwa katika juhudi za kidiplomasia zinazolenga kumaliza vita vya Ukraine, ambavyo vimeendelea tangu Urusi ilipoivamia nchi hiyo Februari 2022.