×

Zambia Yapiga Marufuku Maandamano ya Kupinga Muhula wa Tatu wa Rais Hichilema

LUSAKA, Zambia – Mamlaka nchini Zambia zimepiga marufuku maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Novemba 25, 2026, kupinga mapendekezo ya kuondoa ukomo wa mihula ya urais, hatua iliyozua mjadala kuhusu uhuru wa kujieleza na haki ya wananchi kukusanyika kwa amani nchini humo.

Rais Hakainde Hichilema

Maandamano hayo yaliandaliwa na mashirika ya kiraia pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu waliopinga mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba yanayoweza kumruhusu Rais Hakainde Hichilema kuendelea kugombea urais baada ya mwaka 2031, atakapokamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho kwa mujibu wa Katiba ya sasa.

Polisi walieleza kuwa wamezuia maandamano hayo kutokana na hofu ya kutokea kwa makabiliano kati ya waandamanaji wanaopinga mabadiliko hayo na kundi la vijana wanaounga mkono Serikali, lililotangaza kufanya maandamano ya kuunga mkono kuondolewa kwa ukomo wa mihula ya urais.

Kwa mujibu wa taarifa ya Al Jazeera, mashirika matatu yanayohusishwa na chama tawala cha United Party for National Development (UPND) yamewasilisha maombi Bungeni yakitaka kuondolewa kwa masharti ya ukomo wa mihula ya urais.

 

Hata hivyo, pendekezo hilo limekabiliwa na upinzani kutoka kwa mashirika ya kiraia, Kanisa Katoliki na Chama cha Wanasheria cha Zambia (LAZ), ambao wameeleza wasiwasi wao kuhusu athari zinazoweza kujitokeza endapo ukomo huo utaondolewa.

Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Ndani, Clement Andeleki, ametetea uamuzi wa polisi wa kuzuia maandamano hayo, akisisitiza kuwa Rais Hichilema hana nia ya kutafuta muhula wa tatu wa urais.

Kwa upande wake, Linda Kasonde, aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria cha Zambia na mmoja wa waandaaji wa maandamano hayo, amesema waandaaji wamewasilisha rufaa kwa polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani wakitaka kupangiwa tarehe nyingine ya kufanya maandamano ya amani.

Kasonde amesema waandaaji bado wameazimia kutumia haki yao ya kidemokrasia kueleza upinzani wao dhidi ya mapendekezo ya kuondoa ukomo wa mihula ya urais.

Wakati huohuo, mjadala huo unaendelea kuibua hisia tofauti nchini Zambia, huku wanaounga mkono mabadiliko hayo wakidai kuwa kuondoa ukomo wa mihula kutawapa wapiga kura uhuru mpana wa kuwachagua viongozi wanaowataka, wakati wapinzani wa pendekezo hilo wakisisitiza kuwa ukomo wa mihula ni moja ya misingi muhimu ya kulinda demokrasia na kuzuia mkusanyiko wa madaraka kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Katiba ya sasa, Rais Hichilema, aliyeingia madarakani mwaka 2021, anatarajiwa kumaliza muhula wake wa pili mwaka 2031.

Leave a Comment