
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linawashikilia askari nane wa Maliasili Wilaya ya Mbozi kwa mahojiano kufuatia tukio la ufyatuaji risasi lililosababisha kifo cha mwanafunzi wa darasa la tano, Vanesa Mgala (13), na kumjeruhi mwananchi mwingine katika Kijiji cha Manyara, Wilaya ya Mbozi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Novemba 27, 2026 na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Akama Shabani, tukio hilo lilitokea Novemba 24, mwaka huu, majira ya saa 11 jioni, wakati askari hao walipokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kudhibiti uchomaji wa mkaa katika eneo hilo.
Taarifa inaeleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni zoezi la kuwakamata watu waliokuwa wakikata miti na kuchoma mkaa ndani ya msitu wa Manyara. Hata hivyo, baadhi ya wananchi walidaiwa kuingilia kati na kuwazingira askari hao, hali iliyosababisha kutokea kwa vurugu na hatimaye ufyatuaji risasi.
Katika tukio hilo, Vanesa Mgala alijeruhiwa kwa risasi sehemu ya tumbo na mikononi, huku mwananchi mwingine akijeruhiwa mkono na paja la mguu wa kushoto. Vanesa alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mbozi Mission.
Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi pamoja na kuwahoji askari hao wanane ili kubaini ukweli wa kilichotokea na mazingira yaliyopelekea kutokea kwa tukio hilo, huku likiahidi kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kuhusika.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limetoa wito kwa wananchi kuheshimu mamlaka zinazotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kuepuka vitendo vya vurugu na kuzingatia sheria za nchi.
