×

Exim Tanzania Yachochea Ukuaji wa Uchumi na Ustawi wa Jamii Kupitia Korosho Marathon 2026

Benki ya Exim Tanzania imeendelea kuonesha dhamira yake ya kushiriki katika kukuza maendeleo ya jamii na uchumi wa nchi kupitia udhamini wa mbio za kilomita tano (5KM Fun Run) katika mashindano ya Korosho Marathon 2026 yaliyofanyika Mtwara.

Udhamini huo ni sehemu ya jitihada za benki hiyo kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi, kuzingatia afya bora na kushiriki katika shughuli zinazojenga mshikamano wa kijamii.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Kanda wa Benki ya Exim Tanzania, Emmanuel Sango, amesema benki hiyo inaamini kuwa maendeleo ya jamii hayaishii katika huduma za kifedha pekee, bali yanahusisha pia kuunga mkono shughuli zinazoboresha maisha ya wananchi na kufungua fursa za kiuchumi.

Sango ameeleza kuwa sekta ya korosho ina nafasi kubwa katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Mtwara na wananchi wake, hivyo ni muhimu kuwepo kwa juhudi za pamoja katika kuongeza thamani ya zao hilo kupitia usindikaji, biashara na upanuzi wa masoko.

Ameongeza kuwa huduma za kifedha zina nafasi muhimu katika kuwawezesha wakulima, wafanyabiashara na wadau wengine wa sekta hiyo kukuza shughuli zao, kuongeza uzalishaji na kunufaika zaidi na fursa zinazopatikana katika mnyororo mzima wa thamani wa zao la korosho.

Kupitia ushiriki wake katika Korosho Marathon 2026, Exim Bank Tanzania inalenga kuonesha umuhimu wa kuunganisha afya bora na maendeleo ya kiuchumi, kwa kutambua kuwa jamii yenye afya njema ina nafasi kubwa ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo.

Aidha, udhamini huo unaakisi dhamira ya benki hiyo ya kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhamasisha maendeleo endelevu, kuimarisha mahusiano na jamii pamoja na kuchochea mshikamano kupitia michezo.

Katika kuendeleza mchango wake kwenye sekta ya korosho, Exim Bank Tanzania inaendelea kutoa suluhisho mbalimbali za kifedha zinazolenga kukidhi mahitaji ya wateja wake, hususan wakulima na wafanyabiashara wanaojihusisha na uzalishaji, usindikaji na biashara ya zao hilo.

Hatua hiyo inaendelea kuweka msisitizo katika umuhimu wa sekta ya fedha kushirikiana na wadau wa kilimo na jamii kwa ujumla ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza fursa za biashara na kujenga maendeleo endelevu nchini.

Kupitia Korosho Marathon 2026, Exim Bank Tanzania inaendelea kusisitiza kuwa uwekezaji katika afya ya jamii na uwezeshaji wa kiuchumi ni sehemu muhimu ya safari ya maendeleo.

Leave a Comment