ILIPOISHIA WIKIENDA
Tukaenda kukaa sebuleni. Muda ule ilikuwa ni saa tisa usiku. Tukazungumza hadi saa kumi. Shemeji akaanza kusinzia. Baadaye nikamuona dada naye yuko kimya. Nikajipa moyo kwamba kutakucha muda si mrefu.
Baadaye na mimi nikapitiwa na usingizi hapohapo, nikalala.
Dada ndiye aliyeniamsha kukiwa kumeshakucha.
“Nenda kalale chumbani,” akaniambia.
Nilipotupa macho, shemeji alikuwa ameshaondoka. Nikainuka na kuingia chumbani. Wakati naingia tu chumbani, simu yangu ikaita. Kwa kweli nilishituka kwa kudhani kuwa ni yule jini. Nilipotazama sikrini ya simu nikaona jina la Eddy, mpenzi wangu aliyekuwa masomoni Uingereza.
SASA ENDELEA…
Pia sikuamini kuwa alikuwa ni Eddy kweli. Nikahisi labda yule jini amegeuza namba ili nipokee simu yake. Nikaipokea huku nikiwa na mashaka.
“Hello!” nikasema kwa kutega.
“Hello Baby…”
Naam ilikuwa sauti ya Eddy.
“Mbona unanipigia kwa namba ya Tanzania?” nikamuuliza.
“Nimewasili sasa hivi kutoka London, niko Uwanja wa Ndege wa Dar lakini ninakwenda Zanzibar kwa ndege nyingine.”
“Mbona umekuja ghafla?”
“Tulianza likizo jana ndiyo nikaona nije huku. Unaweza kuja Unguja?”
“Ninaweza.”
“Basi njoo, nitakuwa Hoteli ya Ziwani. Ukinipigia baadaye nitakwambia niko chumba namba ngapi.”
“Sawa. Ninajiandaa nitakapoondoka nitakujulisha.”
“Oke.”
Eddy akakakata simu. Simu ya Eddy ikawa imebadili fikira zangu. Ile hofu niliyokuwa nayo ikaondoka, badala yake nikawa na furaha ya kukutana na mpenzi wangu ambaye nilipoteana naye kwa mwaka mzima alipoondoka kwenda masomoni Uingereza.
Mpaka inafika saa nne nilikuwa nimeshajiandaa kwa safari ya kwenda Zanzibar. Nilimfahamisha dada yangu kuwa nakwenda Zanzibar kwa Eddy.
“Kwani Eddy amerudi?” Dada akaniuliza.
“Amenipigia simu asubuhi akiwa uwanja cha ndege hapa Dar akitokea London, ameniambia nimfuate Zanzibar.”
“Ina maana alipofika tu akaondoka kwenda Zanzibar.”
“Ndiyo, aliondoka kwenda Zanzibar.”
“Basi hizo zawadi za Ulaya usitukose.”
Baada ya hapo nikaenda zangu bandarini. Nilikata tiketi ya boti inayoondoka saa saba. Baada ya kukata tiketi nikampigia Eddy.
“Eddy Vipi?” nikamuuliza alipopokea simu yangu.
“Ndiyo unakuja?” Eddy akaniuliza.
“Niko bandarini. Boti itaondoka saa saba.”
“Ukifika njoo Hoteli ya Ziwani, niko chumba namba 85. Kipo ghorofa ya pili.”
“Sawa.”
Nilikata simu. Mimi na abiria wenzangu tukajipakia kwenye boti.
Safari ilianza saa saba. Tulipofika Unguja nilikodi Bajaj iliyonipeleka Hoteli ya Ziwani. Ilikuwa hoteli kubwa iliyokuwa karibu na ufukwe wa Bahari ya Hindi.
Nilipofika Hoteli ya Ziwani nilishuka kwenye Bajaj nikaingia ndani ya hoteli hiyo. Nilifika mapokezi nikaeleza kwamba kulikuwa na mgeni wangu aliyekuwa chumba namba 85.
“Chumba namba 85 kipo ghorofa ya pili.”
“Sawa.”
Nikapanda ngazi hadi ghorofa ya pili. Nikakitafuta chumba namba 85, nikakiona. Nilikwenda kwenye mlango wa chumba hicho nikabisha lakini sikupata jibu.
Kwa vile mwenyewe alishaniambia kuwa atakuwa katika chumba hicho, nilifungua mlango nikaingia. Nikamuona Eddy akipekua kwenye kabati. Alikuwa amenipa mgongo.
Nikaurusha mkoba wangu kwenye kitanda nikamfuata ili nimkumbatie. Kabla sijamfikia aligeuka akanitazama. Eh! Kumbe hakuwa Eddy. Alikuwa ni yule jini mzungu!
Moyo wangu ulishituka. Nikamuona akitabasamu na kuniambia:
“Karibu.”
Nilikuwa nimeshapeleka mikono yangu nimkumbatie, nikairudisha haraka kisha nikageuka na kurudi kwenye mlango. Niliufungua na kutoka mbio.
“Ah! Balaaa gani hili!” nilijisemea huku nikishuka ngazi harakaharaka.
Nilirudi pale mapokezi nikamuuliza yule msichana:
“Aliyekodi chumba namba 85 alikuwa ni nani?”
Msichana alitazama kwenye kitabu cha wageni kisha akaniambia:
“Ni Eddy.”
“Ni Mzungu au Mzanzibari?”
“Ni Mzanzibari.”
“Mbona nakuta Mzungu?”
“Inawezekana ni mwenzake lakini chumba kimetolewa kwa Eddy.”
Mkoba wangu nilikuwa nimeuacha kule chumbani. Nikatoka nje ya ile hoteli. Nilipotupatupa macho, nikaiona gari ya Eddy ikiwa imeegeshwa katika eneo la kuegesha magari. Nikaifuta. Nilimkuta Eddy amelalia usukani wa gari.
Nikafungua mlango wa dereva na kumuita.
“Eddy!”
Wakati mlango unafunguka nikamuona Eddy anachomoka kwenye mlango na kuanguka chini kama mzigo. Nikawahi kumdaka.
Alikuwa ametoa macho na damu ilikuwa ikimtoka puani na midomoni.
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.