Mshindi wa Urais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein akikabidhiwa Cheti cha Ushindi.
Kila mmoja nchini anajua uchaguzi wa Zanzibar umekwisha lakini pia uchaguzi wa kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam umefanyika salama na kumpata mwenyekiti hicho.
Machi 22, mwaka huu wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake walishuhudia historia mpya kufuatia kumalizika mvutano wa muda mrefu kuhusiana na uchaguzi wa meya wa jiji hilo kwani ndiyo siku meya alipopatikana.
Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam awali ulitawaliwa na malumbano makali ya kisiasa na yaliyosababisha matumizi ya hati bandia ya mahakama ya kuahirishwa uchaguzi huo.
Hata hivyo, tamati ya malumbano hayo ilikuwa Jumanne iliyopita baada ya Isaya Mwita Charles aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya Chadema kutangazwa kuwa mshindi wa kiti hicho cha umeya wa jiji.
Meya huyo alipata ushindi wa kura 84 dhidi ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Yusuph Yenga aliyepata kura 67. Hii ni mara ya kwanza kwa CCM kukubali kushindwa kwenye uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.
Mimi naamini kumalizika kwa uchaguzi huo ni mwanzo wa uchapakazi kwa masilahi ya wananchi wa jiji hilo. Meya mpya wa jiji anatakiwa kutatua kero mbalimbali akishirikiana na viongozi wenzake ili kuleta ufanisi wa jiji hilo. Tunalitambua jiji hilo kama kioo cha Tanzania kutokana na kuwa mji mkuu wa kibiashara, ambapo wageni hutumia kama kielelezo cha Tanzania.

Meya wa jiji la Dar, Isaya Mwita
Naamini kuwa Jiji la Dar es Salaam halipaswi kuwa jiji la kero bali lenye kubeba sura halisi ya Tanzania ikiwa na kila aina ya maendeleo na mafanikio.
Nako Zanzibar Rais wa visiwa hivyo amepatikana katika uchaguzi uliofanyika Jumapili ya Machi 20, mwaka huu, si mwingine ni Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye tayari ameapishwa.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Dk. Shein pamoja na mambo mengine, alitoa tamko la matumaini aliposema: “Ninasema tena hapa uchaguzi umekwisha sasa tufanye kazi ya kuleta maendeleo ya kweli hapa Zanzibar, tunajua haikuwa kazi rahisi kwa ZEC (Tume ya Uchaguzi Zanzibar) kusimamia uchaguzi lakini Mungu ametujalia tumemaliza salama.
“Ninawahakikisha nitaunda serikali makini ambayo itafanya kazi kwelikweli kama ilivyo kauli mbinu ya Rais Dk. John Magufuli ya Hapa Kazi Tu,” alisema Dk. Shein tusubiri utekelezaji wake.
Niwaambie tu wanasiasa kwamba zama za kulumbana na kupoteza muda mwingi kwenye malumbano sasa zimekwisha. Nadiriki kuwakumbusha kuwa wakati wa kuchapakazi umefika.
Niwasihi wananchi wote, wale wa Zanzibar na wakazi wa Dar, kwamba tushirikiane na waliochaguliwa kujenga nchi yetu, bila kufanya hivyo tutakuwa tunajidanganya, siku zote umoja ni nguvu, anayepinga hilo si muungwana.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli