The House of Favourite Newspapers

Enzi Zetu, Mwenye Mpira Hakabwi!

0

Enzi hizo wakati bado ningali mtoto, kila mtaa ulikuwa na kiwanja cha kuchezea, tena kikubwa maana unaweza ukakuta michezo mitatu ya soka na miwili ya netiboli inaendelea kwa wakati mmoja, achana na wale waliokuwa wakicheza mdako, kiboleni, gololi na hata kufukuzana tu.

Kwenye soka enzi zile, tulikuwa na sheria zetu za kuongoza mchezo huo. Sheria zetu hazikuwa zinafuata za FIFA, kwanza wakati huo hata hilo neno FIFA tulikuwa hatulijui. Wenyewe tulijitengenezea amri ambazo hazikuandikwa popote lakini kila mtu alikuwa anazijua kimoyomoyo.
Tulikuwa na amri zetu kama kumi hivi. Kwanza wakati huo mipira yenyewe ilikuwa tabu kupatikana hivyo wengi tulikuwa tunatengeneza wenyewe kwa kufunga makaratasi na kuanza mechi ambazo kupumzika ni uamuzi tu, inawezekana mtu kishafungwa 20 kwa kumi na mbili, basi mnaamua kupumzika.

Lakini ilikuwa ikitokea mwenzenu mmoja wazazi wake wako vizuri wakamnunulia mpira wa kweli, hapo basi kidogo kulikuwa na taratibu mpya katika kuchezea mpira ule. Tulijitengenezea  amri kama kumi hivi. Amri ya kwanza ilikuwa mwenye mpira ndiye anayeamua nani atacheza, hivyo kama uliwahi kumnyima kashata au andazi ni wazi huchezi.
Amri ya pili ilikuwa mtoto bonge ndiye golikipa, hilo lilikuwa halina ubishi. Tatu ni kuwa wachezaji wazuri ndiyo wanaochaguliwa kwanza na mwenye mpira kuwa watakuwa timu yake. Amri ya nne ilikuwa kukiwa na penati ruksa kubadilisha kipa kama kipa wenu hamumuamini.

Amri ya tano ya mpira enzi zetu ni kuwa ukipiga mpira kwa nguvu au kwa mandochi yaani kwa vidole, kumbuka tulikuwa hatuvai viatu, basi mwenye mpira ana ruksa ya kukuonya au kukukataza usicheze. Amri ya sita ya mpira enzi zetu ni kuwa usipochagia hela ya kujaza upepo mpira utapigwa marufuku kucheza.
Amri ya saba ilikuwa hakuna marefa wala washika vibendera na mpira unachezwa mpaka kuzunguka goli, ila mwenye mpira anaweza akageuka refa wakati wowote na atakachosema lazima kiwe. Kati ya amri muhimu ilikuwa ni ile ya nane, si ruhusa kabisa kumkaba mwenye mpira, hiyo ni faulo.
Ya tisa ni kuwa ukitoboa mpira unalipa. Mwisho ni kuwa mwenye mpira akikasirika au akiumia au akiitwa na mama yake ndiyo mwisho wa mechi.

Leave A Reply