
Mkuu wa Wilaya ya Geita – Manzie Mangachie (kushoto) akimpongeza Meneja Mwandamizi wa Mitandao ya Matawi ya NMB – Gabriel Ole-Loibanguti kwenye hafla ya kufungua rasmi tawi la NMB Katoro. Tawi hili linafanya NMB kufikisha jumla ya Matawi 176 nchi nzima na ATM zaidi ya 600 na kuifanya benki hiyo kuwafikia watanzania wengi zaidi na wa hali zote mijini na vijijini. Anayeshuhudia ni Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa – Abraham Augustino.

Afisa Tawala wa Wilaya ya Tarime – John Marwa (wa pili kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Tawi la NMB Nyamongo wilayani Tarime mkoani Mara. Tawi hili linafanya NMB kufikisha jumla ya Matawi 176 nchi nzima na ATM zaidi ya 600 na kuifanya benki hiyo kuwafikia watanzania wengi zaidi na wa hali zote mijini na vijijini. Kulia ni meneja wa NMB kanda ya Ziwa – Abraham Augustino na kushoto ni Meneja Mwandamizi wa Mitandao ya Matawi ya NMB – Gabriel Ole-Loibanguti na Paul Kangele Meneja wa tawi la NMB Nyamongo.
- Wateja zaidi ya 300 kupata huduma kila siku katika Matawi hayo
Kanda ya Ziwa Machi 22, 2016… Benki ya NMB imefungua matawi mawili ya NMB Katoro na NMB Nyamongo kanda ya ziwa katika mikoa ya Geita na Mara na kufanya jumla ya matawi ya NMB kanda ya ziwa kwa mikoa ya Mara, Mwanza, Geita na Kagera kufikia matawi ishirini na nne.
NMB imekua ikiongeza matawi mengi katika azma yake ya kuwafikia watanzania wote na kuendelea kuwa benki yenye matawi mengi zaidi nchini ambayo mpaka sasa imefikisha matawi 176 na ATM zaidi ya 600 nchi nzima huku ikijivunia uwepo katika kila wilaya nchini.
Matawi hayo mapya ya NMB Nyamongo na NMB Katoro kwa pamoja yanahudumia watanzania zaidi ya 600 kila siku huku ikiwapunguzia adha wananchi wa maeneo hayo ambao wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za kibenki. Wakazi wa Nyamongo walikuwa wanasafiri mpaka Tarime kupata huduma za kibenki huku wale wa Katoro mpaka waende Geita ambapo ndiko kulikokuwa na matawi ya benki.
Maeneo yote haya yanakaliwa na wafanya biashara zaidi na wavuvi ambao huduma za kibenki kwao limekuwa ni jambo muhimu sana ili kuondoa uwezekano wa kutuza fedha majumbani na hivyo kuhatarisha maisha yao kutokana na ujambazi.
Akizungumza katika ufunguzi matawi haya, Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa – Abraham Augustino alisema lengo kubwa la kupeleka matawi hayo ni kuwapa huduma kwa ukaribu wateja wao waliopo katika maeneo hayo husika. Alifafanua kwamba, tangu kuanzishwa kwa matawi hayo yamekuwa ni mkombozi kwa wateja wengi wakiwemo wafanyabiashara wakubwa na wadogo pamoja na watu mbalimbali.
“Matawi yetu yanatoa huduma zote za kibenki, na tunazidi kuwakaribisha wateja wetu ili wajionee huduma bora zitolewazo na benki yetu na pia tunatoa huduma mbalimbali zikiwemo za Mashine za kutolea fedha(ATM) ambayo hufanya kazi kwa masaa 24”. Alisema Abraham
Mkuu wa Wilaya ya Geita – Manzie Mangachie alisema kuwa NMB imekuwa mkombozi wa watanzania hivyo kuwataka wana Geita kuitumia benki hiyo kwa ukamilifu ili kupata faida zinazotokana na huduma za NMB.
“NMB imekuwa karibu sana na wananchi si tu kwa kutoa huduma za kibenki bali hata kuungana na watanzania wengine katika kutatua shida zao kwa kuwapatia madawati mashuleni, vifaa vya hospitali ambavyo vimekuwa vikitumiwa na watu wote wateja wa NMB n ahata wasio wateja, “ alisema Mangachie.