×

Sitasahau Nilivyokumbana na Jini Mwanaume-13

ILIPOISHIA IJUMAA:
Vile nilivyokuwa nimeduwaa nikiitazama, ile simu ilijipokea yenyewe ikajiongezea sauti. Nikaisikia sauti ya Smith ikiniambia.
“Kama unajaribu kunikimbia mimi utapata matatizo mengi.”
Sikujibu kitu, nikanyamaza kimya huku nikijiona wazi kuwa nilikuwa natetemeka.
“Hivi sasa polisi wanakutafuta kwa mauaji ya Eddy na Eddy nilimuua mimi kwa sababu uliniambia huna mpenzi,” sauti ya Smith ikaendelea kuniambia.
Nikaendelea kunyamaza.
“Usalama wako ni kuwa na mimi. Ukiwa na mimi matatizo yote yatakwisha na kesi yako ya Zanzibar pia itakwisha. Sasa niambie kama uko tayari kuwa na mimi.”
SASA ENDELEA…

Maneno ya yule jini yalikuwa yanauma kwenye moyo wangu. Mbali na kuuma, pia yalikuwa yamenipa mchanganyiko wa shauku na hofu.
Yalinipa shauku ya kutaka kuyasikiliza kwa sababu yalinifahamisha kile nilichokuwa nataka kukijua kuhusu Eddy. Sasa nilikwishajua na kupata uhakika kwamba Eddy ameuawa na Smith na ameuawa kwa sababu alikuwa mpenzi wangu.
Pia nilishajua kwamba polisi wa Zanzibar walikuwa wakinitafuta kwa tuhuma ya mauaji ya Eddy.

Lakini shauku yangu ilikuwa imechanganyikana na hofu ya kukamatwa na polisi na pengine nishitakiwe mimi kwa mauaji ya Eddy. Na pia nilikuwa na hofu ya kuandamwa na yule jini kiasi kwamba sasa alikuwa ameyaingilia maisha yangu na kutishia kuyaweka hatarini.

Wakati nikiwaza hayo, sauti ya Smith ilikuwa ikiendelea kusikika kwenye simu.
“Enjo usijidanganye kuwa utaweza kunikimbia mimi au kunidanganya kwa sababu ninakufahamu vizuri na nimeshashika kivuli chako. Ulikubali mwenyewe kuwa utanipenda, sitakuachia ufanye vinginevyo hata kidogo,” sauti ya Smith iliniambia.
“Naomba unisamehe…!” nikashtukia nikisema hivyo huku nikianza kulia kwa hofu.
“Nikusamehe nini?” Smith akaniuliza kwenye simu.
“Mimi nimekuona wewe uko tofauti ndiyo maana nimekukimbia.”
Niliposema hivyo nikaisikia sauti ya kicheko ya Smith. Lakini niligundua kilikuwa kicheko cha uongo.

“Oh! Kwa nini una hofu? Nilitaka kukuonesha kuwa umepata mpenzi wa kijini ambaye atakupa utajiri…” akaniambia baada ya kicheko.
“Kumbe wewe ni jini?” nikamuuliza baada ya kukiri yeye mwenyewe kuwa ni jini.
“Ndiyo, mimi ni jini kama ulivyoniona lakini usiogope utanizoea tu.”
“Sasa mimi sitaki tena urafiki na wewe.”
“Haitawezekana kwa sababu nimeshakupenda, lazima ukubaliane na mimi, vinginevyo utapata matatizo.”
“Mama yangu! Mimi najuta sasa…mimi siwezi kuwa na mpenzi kama wewe. Naomba unisamehe.”
“Majini wengi wana wapenzi binadamu na wanawapa utajiri. Wewe hutaki utajiri?”
“Sitaki.”
“Sikiliza Enjo, mimi naweza kuharibu maisha yako mara moja….” Sasa sauti yake ilikuwa imebadilika.
“Mama yangu wee…!”
Maneno ya jini huyo yalizidi kunitia hofu na sikutaka kuyasikiliza tena. Nikabonyeza kitufe cha kukata mawasiliano. Lakini mawasiliano hayakukatika. Nilikiminya tena na tena kitufe hicho bila mafanikio.

Nikaona sasa nifungue simu nitoe betri. Huku Smith akiendelea kunitishia, niliifungua simu harakaharaka, nikafanikiwa kuchomoa betri na hapohapo simu ikazima. Kitendo hicho kilinifanya niheme kama niliyekuwa nimefanya kazi kubwa.

Nikaendelea kuangaza macho yangu kila upande kulitazamia gari la shemeji. Gari sikuliona. Nikatamani nimpigie simu dada lakini nisingeweza tena kwa sababu betri nilishaitoa.
Nikabaki nimechanganyikiwa.

Ghafla nikaliona gari hilo. Nikakurupuka kulifuata huku nikilipungia mkono. Sikujali kuwa nilikuwa nimetokeza barabarani ambako ningeweza kugongwa na gari lingine.
Shemeji akaniona, akafunga breki. Nikakimbilia kwenye mlango wa upande wa pili wa dereva nikaufungua na kujipakia harakaharaka.

“Nilikuwa nakupigia simu nikuulize uko kwa wapi, naona simu haipatikani,” shemeji akaniambia.
Kabla sijamjibu, shemeji akauona uso wangu. Akaniuliza.
“Ulikuwa unalia?”
Nilijifuta uso kwa mikono. Ile kwikwi ya kilio ilinifanya nisiweze kumjibu chochote. Shemeji akaliondoa gari.
“Mbona sikuelewi Enjo. Naona simu umeifungua, betri iko mbali halafu uko kivingine kama ambaye hutoki safari. Mkoba wako uko wapi?”
“Ni makubwa shem, wewe acha tufike nyumbani. Siwezi kukueleza ndani ya gari.”
Shemeji akanielewa. Hakuniuliza kitu tena.
Tulipofika nyumbani ndipo nilipoeleza yaliyonikuta. Nilianzia yale ya Zanzibar, nikamalizia na ile simu aliyonipigia Smith.

Dada na mume wake wakashangaa.
“Ndiyo maana nikakukuta unalia?” Shemeji akaniuliza.
“Nisilie, unayaona hayo ni madogo!” nikamuuliza.
“Kwa kweli ni makubwa.”
“Lakini Enjo mdogo wangu, matatizo uliyataka mwenyewe, kwa nini mtu anakutongoza unamkubali wakati hamjuani?” Dada akaanza kunilaumu.

Je, kiliendelea nini? Usikose mwendelezo wa mchirizi huu katika Gazeti la Ijumaa siku ya Ijumaa.

Leave a Comment