Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa, anaponea chupuchupu kufa katika ajali ya kutengenezwa.
Anaokolewa na jasusi wa kimataifa, Grace ambaye anatumia utaalamu wa hali ya juu na kuwafanya watu wote waamini kwamba amekufa. Wawili hao wanatorokea mafichoni ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.
Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi. Tayari baadhi ya mambo yameanza kufichuka ambapo inaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya kifo cha Mwampashi na Magesa.
Kaburi ambalo kila mtu anaamini kwamba ndipo alipozikwa Magesa, linafukuliwa na sampuli zinachukuliwa kwa ajili ya vipimo vya DNA. Baadaye inabainika kwamba aliyezikwa hakuwa Magesa bali mtu mwingine tofauti kabisa.
Kadiri upelelezi unavyozidi kupamba moto ndivyo mambo mengi yanavyozidi kuibuka na sasa watu wengine wanahojiwa kuutafuta ukweli wa tukio zima. Sekretari wa Magesa na yule wa waziri mkuu nao wanahojiwa ambapo mambo ya ajabu yanazidi kubainika na sasa ipo wazi kwamba kuna mkono wa waziri mkuu.
Jitihada za kumfikisha kwenye mikono ya sheria zinazidi kupamba moto lakini ghafla Mandiba anajikuta akiwa matatizoni baada ya kugundua kuna watu wanamfuatilia. Ananusurika kuuawa baada ya kutumia mbinu za hali ya juu za kijeshi lakini bado jinamizi linaendelea kumuandama na sasa anajikuta kwenye matatizo mengine.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Mandiba alienda moja kwa moja kwenye chumba cha kuongozea kamera za usalama. Akisaidiana na mganga mkuu pamoja na mtaalamu wa teknolojia ya mawasiliano hospitalini hapo, walianza kufuatilia kamera zote na kurudisha nyuma picha za matukio yaliyotokea kwa kipindi cha nusu saa iliyopita.
“Hebu simamisha hapo,” alisema Mandiba baada ya kubaini kwamba kuna kipande katika rekodi ya matukio yote, kilikuwa kikionesha giza, yule mtaalamu wa teknolojia ya mawasiliano hospitalini hapo akafanya kama alivyoambiwa.
“Kwa nini hapa hakuna picha zinazoonekana? Tena ni kwa kamera zote?”
“Kuna muda huwa inatokea, unajua umeme wetu hapa siyo wa uhakika kwa hiyo inapotokea hitilafu hata ndogo tu, kamera huwa zinajizima,” alisema mtaalamu yule, kauli iliyomfanya Mandiba ashindwe kabisa kumuelewa.
Hata hivyo, waliamua kuendelea kufuatilia picha hizo za matukio yote lakini tukio lililoonekana ni lile la Mandiba kuingia ndani ya wodi hiyo na kuonekana akizungumza na mgonjwa huyo ambaye hakuwa na uwezo wa kumjibu chochote zaidi ya kumuonesha lugha ya ishara.
Walirudia zaidi ya mara kadhaa kutafuta video zilizomuonesha mtu huyo akiingia wodini lakini hazikupatikana.
“Hapa kuna mchezo mnataka kunichezea, nimeshajua,” alisema Mandiba, akachomoa simu yake mfukoni na kuanza kupiga upande wa pili. Alishaelewa nini kingetokea endapo jambazi yule angekufa.
“Grace! Im in great troubles, it seems the guy is trying to stop me in a very hard way! Im due to be accussed of murder!” (Grace, nipo kwenye matatizo makubwa, inaonesha huyu jamaa anatumia nguvu kubwa sana kunizuia nisiendelee kumfuatilia, muda si mrefu nitakuwa nakabiliwa na kesi ya mauaji) alisema Mandiba baada ya upande wa pili kupokea simu.
Kabla hata hajamaliza kuzungumza na simu hiyo, akiwa kwenye korido na yule mtaalamu wa teknolojia ya mawasiliano, wakitoka kwenye chumba cha kuongozea kamera za ulinzi (CCTV), Mandiba alishtukia akizingirwa na maafisa kadhaa wa jeshi la polisi aliokuwa akifahamiana nao vyema kwa sababu walishafanya kazi pamoja mara kadhaa.
“Mkuu samahani kuna tatizo limetokea, nimeagizwa unikabidhi kitambulisho chako na bastola kisha uongozane na hawa askari,” Alfred Lupenza, msaidizi wa Mandiba aliyekuwa ameongozana na wale askari, alimwambia bosi wake.
“Nani amekutuma Lupenza? Halafu mnaniweka chini ya ulinzi kwa kosa gani?”
“Unahusishwa na mauaji ya mgonjwa aliyekuwa amelazwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi chini ya ulinzi mkali. Haya ni maagizo kutoka juu, naomba utusamehe,” alisema askari mwingine aliyekuwa kwenye kundi lile, aliyeonesha kuwa na mamlaka kuliko wenzake.
Mandiba alishusha pumzi ndefu na kwa sababu alishaelewa ni nini kilichokuwa kinaendelea, alimtazana Lupenza kisha akamtazama yule kiongozi wa wale askari, akatoa kitambulisho chake na bastola ndogo iliyokuwa kiunoni, akamkabidhi Lupenza kisha akanyoosha mikono yake ili afungwe pingu.
Askari mmoja akachomoa pingu kiunoni na kumfunga mikononi, kwa mbele na kumpa ishara kwamba awafuate. Mandiba hakuwa mbishi, alifuatana na maafisa hao wa polisi na wakiwa wanakaribia kwenye wodi aliyokuwa amelazwa yule jambazi, walishuhudia kitanda cha magurudumu kikisukumwa kutolewa nje ya wodi, huku juu yake kukiwa na mwili uliofunikwa kwa shuka la rangi ya kijani.
Haukuwa utaratibu wa kitabibu wa mtu kutolewa wodini muda mfupi kiasi hicho baada ya kufariki, Mandiba akazidi kupata uhakika kwamba kuna njama zinaendelea. Wakati akitolewa nje, polisi wengi wakiwa wametanda kila mahali, alizingirwa na waandishi wa habari ambao hata hakuelewa wamepata wapi habari za tukio hilo wakati hata dakika tano hazikuwa zimepita.
Akawa anapigwa picha nyingi huku wengine wakimsogelea na kumhoji maswali yaliyomshangaza sana.
“Ni kweli mheshimiwa umeamua kulipa kisasi kwa kumuua mtu aliyetaka kukuua usiku nyumbani kwako?”
“Mkuu kwa nini hukusubiri sheria ichukue mkondo wako mpaka umeamua kumuua mwenyewe kwa mikono yako,” yalikuwa ni baadhi ya maswali kutoka kwa waandishi wa habari waliokuwa wakimzonga kila sehemu.
Mwenyewe hakutaka kujibu chochote, akaongozwa mpaka kwenye gari la polisi lililokuwa pale nje, akiwa anataka kuingia, macho yake yaligongana na mheshimiwa waziri mkuu ambaye kumbe naye alikuwepo eneo lile, wakatazamana kwa sekunde kadhaa kisha Mandiba akaingia ndani ya gari na kuondolewa eneo hilo akiwa chini ya ulinzi mkali.
Muda mfupi baadaye, vyombo vingi vya habari vilikuwa vikiripoti tukio hilo lakini tofauti na ukweli ulivyokuwa, wengi walikuwa wakieleza kwamba Mandiba amekamatwa na polisi baada ya kwenda kulipa kisasi hospitali kwa jambazi aliyemvamia na wenzake nyumbani kwake.
Wengine walieleza kwamba amefanya mauaji ya watu wawili, mmoja kwa kumgonga na gari na mwingine kwa kumwekea sumu kwenye dripu, kila mtu alizungumza lake na kuzua gumzo kubwa mitaani. Ni watu wachache tu, wenye uwezo wa kuchanganua mambo ndiyo waliohisi kwamba huenda kuna mchezo uliokuwa ukiendelea nyuma ya pazia.
Tukio lililomtokea Mandiba, kuanzia kunusurika kuuawa usiku nje ya geti la nyumba yake mpaka kukamatwa kwa kesi nzito ya mauaji, viliwafanya wenzake waliokuwa wakishirikiana kutaka kuhakikisha mhusika wa ‘mauaji’ ya Magesa na Mwampashi anafikishwa mbele ya sheria, waingiwe na hofu kubwa ndani ya mioyo yao.
Ilikuwa wazi kwamba baada ya mwenzao kunaswa kwenye mtego hatari, ni wao ndiyo waliokuwa wanafuatia, jambo lililowapa wasiwasi mkubwa ndani ya mioyo yao. Mtu pekee ambaye walikuwa wakimtegemea kwa wakati huo, hakuwa mwingine bali Grace ambaye naye hawakuwa wakijua yupo wapi na wanawezaje kumpata kwa urahisi.
Kwa mheshimiwa waziri mkuu, huo ulikuwa ushindi mkubwa kwake kwani aliamini baada ya kumdhibiti Mandiba ambaye kwake ndiye aliyekuwa hatari kuliko wenzake, alikuwa amefanikiwa kuzima sakata zima, akaendelea kutengeneza njama ili ionekane kweli Mandiba alihusika kumuua mtu yule wodini.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne ijayo kwenye Gazeti la Uwazi.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW
INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/
TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari
FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers
YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1
upo vzr shigo