Asalam alaikum wapenzi wasomaji wa safu hii, bila shaka mko poa mnaendelea vema na ujenzi wa taifa letu, tunashukuru Mungu ametupunguzia joto maana lilikuwa kero kila kona kwani hata ungetumia feni bado ilikuwa shida.
Joto hilo ndiyo limenipa mada ya kuongelea siku ya leo kwani wapo waliolitumia kuanika miili yao na kuharibu ndoa zao kwa kuwatamanisha wanaume wengine.
Juzi baada ya kutoa mada iliyopita, nilipata ujumbe kutoka kwa msomaji wangu, yeye alisema kuwa ameingia kwenye mgogoro na mke wake kwa sababu ya mavazi anayovaa kwa sasa lakini akimuuliza anamwambia joto ndiyo sababu ya yeye kuacha maungo yake wazi.
Wasomaji hii si sawa na kwa kutumia ukurasa huu nimeamua kuwakumbusha wanawake wenzangu kuijua thamani ya mwili wako na kujua thamani ya ndoa uliyonayo kuwa haitakiwi kile mumeo anachokiona kila mtu akione hata kama kuna joto kiasi gani huwezi kuvaa kanga moja na kwenda mtaani au kupita mbele ya mashemeji zako kwa kusingizia joto.
Mwanamke unatakiwa kujipanga, kuna mavazi ya kujistiri kabisa ambayo hata kwenye joto unaweza kuyavaa na siku ikaisha bila kuvaa kanga moja, hivi hili joto tunaloliongelea limeanza leo au ni mtu kuamua kujirahisisha tu na kisingizio kiwe joto.
Wanawake haohao utakuta anamshindisha mtoto wa kike na nguo ya ndani tu na wakati mwingine anatembea naye mtaani ukimuuliza mbona huyu mtoto hajavaa anakwambia we.. mwanangu akivaa anaharibika mwili.
Huoni kuwa wewe ndiyo unachangia kwa kiasi kikubwa kumharibu mtoto? Atakapozoea kukaa utupu itakuwa hivyo hata akikua mavazi yake yatakuwa kama ya mastaa wa mjini ambao wanakwambia wao hawavai nguo za ndani huku wengine wakitembea nusu utupu kisa tu malezi.
Nakukumbusha mwanamke mwenzangu asili yetu ni kujifunika, unaambiwa kitu kinachofunikwa siku zote ndicho huwapa hamu watu kukifunua na wakati mwingine kukionja, sasa wewe unayejiacha wazi nani atakuthamini? Atakuangalia, atakuchoka mapema.
Asikwambie mtu unaweza kumchosha mumeo kwa kujiachia mtupu kwa watu kila siku maana kila jirani atamwambia alama uliyonayo mwilini wakati yeye ndiyo alitakiwa kuijua unadhani atakuwa na hamu ya kuendelea kuwa na wewe? Mwanamke tafakari kabla ya kuamua vazi unalovaa lifikirie mara mbili je linafaa je, hadhi yangu haitashuka kwa kulivaa vazi hili, ukishafanikiwa sasa vaa kwani majibu yote utakuwa nayo.
Kwa leo naishia hapo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada motomoto.