×

Jini Mweusi – 77

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.
Aliyekuwa akiua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.

Aliamua kukimbia kupitia Mlandizi, huko, akapitia misukosuko mingi na mwisho wa siku akajikuta amefika kwa mzee ambaye anamwambia kwamba angemsaidia kufika Mwanza Mjini ila si kwa miguu kama aliyotaka yeye.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
M
zee yule aliyeitwa Saidi akashangaa, hakuamini alichokisikia kwamba kijana huyo, Dickson alikuwa njiani kuelekea Mwanza, tena kwa miguu. Alimwangalia mara mbilimbili, hakuamini, alimuonea huruma kwani kutoka hapo Dakawa, Morogoro mpaka Mwanza ilikuwa mbali mno.
Njia nzima ya kwenda Mwanza haikuwa salama, hapo walikuwa Dakawa ambapo ilikuwa ndani ya Mbuga ya Wanyama ya Mikumi, hivyo kutoka hapo na kusonga mbele ingekuwa safari ndefu ambayo ingehatarisha maisha yake.

Hakuwa na jinsi, alifikiri kwamba mtu huyo hakuwa na nauli ya kupanda basi, alitaka kumsaidia kiasi fulani cha nauli lakini hakuona kama kuna haja ya kufanya hivyo kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa na usafiri wake, Land Rover Defenders iliyochoka, hivyo kwa kutumia usafiri huo, alitegemea kumfikisha salama mpaka Morogoro Mjini.
“Nitakusaidia kufika Morogoro Mjini,” alisema mzee Saidi.
“Kivipi?”
“Nina usafiri wangu, wala usijali kuhusu hilo,” alisema mzee huyo.
“Hapana! Acha tu niendelee na safari, natumaini nitafika salama,” alisema Dickson.
“Hapana! Njia hii ni hatari sana, kuna wanyama wakali, kuna watu wengi walishawahi kuliwa na simba, chui, sipendi wewe ukutane nao, naomba nikusaidie, hata kama huna nauli, nitakupa mimi,” alisema mzee Saidi, alimuonea huruma Dickson, maisha yake yalikuwa porini tu, hata kumfahamu, hakumfahamu.

Hakutaka kumuona Dickson akiondoka kwa miguu kuelekea Mwanza, alijua hatari iliyokuwepo njiani, kulikuwa na watu wengi walikuwa wakiuawa, kulikuwa na wanyama wakali, hata wafanyakazi wa mbugani nao hawakutaka kabisa kutembea mbugani pasipo gari, walijua hatari iliyokuwepo.
Baada ya kumbembeleza sana Dickson, hatimaye akakubaliana naye kwamba wapande gari lake na kuelekea Morogoro Mjini ambapo huko angechukua basi na kuelekea Mwanza.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, walichokifanya ni kuingia ndani ya gari hilo na moja kwa moja safari kuanza. Njiani, walikuwa wakizungumza mambo mengi, kwa Dickson, japokuwa alijitahidi sana kuuweka uso wake kuwa kwenye tabasamu pana lakini bado hakuwa na amani kabisa.

Morogoro Mjini palikuwa kama Dar es Salaam, kulikuwa na magazeti mengi, mitaani watu walijaa na huko pia picha zake zilibandikwa kila kona kwamba alikuwa akitafutwa kwa udi na uvumba, awe hai au amekufa, bado alihitajika.
Kutoka hapo Dakawa mpaka Morogoro Mjini walitumia saa kadhaa ndipo wakafika ambapo kitu cha kwanza kabisa, Dickson akahitaji kofia kubwa ya Marlboro kwa kisingizio cha kuwa na tatizo kichwani mwake ambapo kama angepigwa sana na jua basi damu zingemtoka puani.

“Nina tatizo la kutoka damu puani, ngoja ninunue kofia,” alisema Dickson, alikuwa akimwambia mzee Saidi. Hilo halikuwa tatizo, kofia ikanunuliwa na kupewa.
Kidogo akawa na amani, aliishusha kiasi kwamba sura yake haikuwa ikionekana vizuri. Kabla ya kwenda Msamvu, wakapitia katika mgahawa mmoja kwa ajili ya kupata chakula cha mchana kabla ya Dickson kuanza safari ya kwenda Dodoma na kuunganisha mpaka Mwanza.

“Hivi huko Mwanza unakwenda kufanya nini?” aliuliza mzee Saidi.
“Nani? Mimi?” aliuliza Dickson japokuwa alilisika sana swali hilo.
“Ndiyo!”
“Nakwenda kuishi huko. Nilikuja Dar mwaka juzi, lengo kubwa lilikuwa ni kutafuta maisha lakini mambo yamekuwa magumu sana, Dar hakuna maisha kama nilivyokuwa nikifikiria kabla, nilidhani kwamba kama ningepata maisha mazuri ndani ya miezi michache lakini hakuna kitu. Sasa si bora nirudi nyumbani nikavue sato na sangara tu,” alisema Dickson.

“Daah! Pole sana. Umechukua uamuzi mzuri sana, kama vijana wengine wangekuwa na uamuzi kama huo, ingekuwa safi sana. Ngoja nikwambie kitu Fabian, vijana wengi wamekuwa hawajiamini, wanahisi kwamba wakienda mjini ndipo watapata maisha mazuri, hakuna kitu kama hicho, wangapi wapo mjini na hawana maisha mazuri? Wapo, tena wengi tu. Nyie kama vijana inabidi mtumie fursa ambazo zipo kila kona, hata vijijini, kote kuna fursa,” alisema mzee Saidi.

Wakati wanazungumza hayo, watu walikuwa wakiingia na kutoka katika mgahawa huo, muda mwingi Dickson alikuwa mtu wa kuangalia chini tu, hakutaka kugundulika kwani kama watu wangejua kuwa alikuwa yeye angekamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Dakika ziliendelea kwenda mbele, wateja waliendelea kumiminika ndani ya mgahawa huo. Dickson akaanza kukosa amani, kitendo cha wateja wengi kujaa humo ndani kilimfanya kuona angekamatwa muda wowote ule. Alichokifanya ni kula haraka ili arudi garini.

“Unakwenda wapi?” aliuliza mzee Saidi mara baada ya kumuona Dickson akiwa amesimama.
“Garini! Nimeshamaliza kula.”
“Sawa! Nenda, nitakuja, ngoja nimalize kula,” alisema mzee Saidi aliyekuwa akila taratibu sana.
Dickson akaondoka ndani ya mgahawa ule na kurudi garini. Alipokuwa akitembea, muda wote macho yake yalikuwa chini kama mtu aliyekuwa akitafuta kitu fulani, picha zake zilisambazwa kila kona, alipoziona, moyo wake ukapiga paaa! Sehemu hiyo haikuwa salama katika maisha yake hata mara moja, alipofika ndani ya gari, akatulia.
Huku nyuma, mzee Saidi aliendelea kula, hakuwa na wasiwasi wowote ule, alichokijua ni kwamba mtu aliyekuwa amemsaidia alikuwa mwema ambaye kwa namna moja au nyingine alihitaji msaada wake.
Alipomaliza, akamuita mhudumu kisha kumlipa. Wakati alipokuwa akitoka, macho yake yakatua katika picha moja iliyobandikwa mlangoni, alitaka kuipita pasipo kuiangalia lakini kitu cha ajabu kabisa kilichotokea, akajikuta akivutiwa kuiangalia picha ile. Alichokiona, hakuamini.

Ilikuwa ni picha ya Dickson, mwanaume aliyekuwa akitafutwa baada ya kufanya mauaji jijini Dar es Salaam, mwanaume aliyekuwa amewaua wanawake wengi na wengine kuwazika, mzee Saidi hakuamini, akasogea karibu kuiangalia picha ile, kweli alikuwa Dickson, mwanaume yuleyule aliyemwambia atangulie garini.
“Kumbe ni muuaji! Milioni ishirini kwa atakayefanikisha kupatikana, haiwezekani, siamini macho yangu,” alisema mzee Saidi, hakuamini, kiasi kilichokuwa kimewekwa kilikuwa kikubwa mno, alikitaka sana hivyo hata kumkamata Dickson hakukuwa na tatizo lolote lile.

Akaondoka hapo mgahawani na kuwahi kule garini, alitaka atakapofika, amdhibiti na kama akishindwa basi apige kelele, wananchi wakusanyike na hatimaye kumkamata. Wakati akielekea kule alipoegesha gari lake, alijiona kama anachelewa kufika, alitamani apate mbawa apae kwani furaha aliyokuwa nayo moyoni, haikuelezeka.
“Amekwisha…” alijisemea mzee Saidi. Tayari mbele yake akajiona kuwa na mamilioni katika akaunti yake benki.
Je, nini kitaendelea? Usikose toleo lijalo.

Leave a Comment