×

Haya Ndiyo Niliyoyaona Baharini-10

ILIPOISHIA GAZETI LA AMANI JANA:
Ndani ya duka lile, tulikutana na wanawake watatu, kama Waraabu hivi, walivaa baibui ambao nao walikuwa wakinunua nguo za kike. Mwanamke mmoja akaniangalia sana kisha akaniambia: “Wewe nakufahamu ni Mtazania, unaitwaaa…”
SASA ENDELEA MWENYEWE…


Juma Ally au bwana Tolu,” Nurdin alidakia kusema bila kumjua yule mwanamke ni nani kwangu.
Alipaswa kuniangalia mimi kwanza kama naonesha kuwafahamu au la!
“Eee! Tolu au Jumaa. Hilo la Juma Ally silikumbuki sawasawa, lakini la Tolu na Jumaa si geni kwangu. Mimi naitwa Bi. Sheila, natokea Dar es Salaam,” alisema yule mwanamke huku wenzake wakiniangalia na kutingisha kichwa kwamba anachosema mwenzao ni sawasawa.

Nilijilazimisha kulikumbuka jina la Bi. Sheila hata halikuwepo kichwani mwangu. Mtihani wa mwisho ukawa ni sehemu gani ya Dar ambayo anaishi Bi. Sheila.
“Dar sehemu gani?” nilimuuliza nikiwa namwangalia kwa macho ya wasiwasi.
“Ilala Mtaa wa Songea.”
Nilishtuka zaidi kwani mimi kwa Dar natokea Mtaa wa Lindi, lakini ni Ilala hiyohiyo. Ni maeneo ya jirani tu. Kwa hiyo nikaanza kumwamini kwamba, kweli ananijua hasa nilipounganisha na kunijua kwa jina la Tolu au Jumaa.
“Umekuja kufanya nini huku Papua New Guinea, mbona ni mbali sana na nyumbani Tanzania?” aliniuliza Bi. Sheila.
“Nafanya kazi kwenye Meli ya Cape.”
“Aaa! Ile ambayo nahodha wake ni Mgiriki anaitwa Sudesdi?”
Kabla sijamjibu nilimwona Nurdin akinikonyeza kama aliyetaka tuondoke eneo lile, nikamkubalia yule mwanamke kisha nikamuaga kwamba sisi tunaondoka.

Tulipofika nje tu, Nurdin akaniambia:
“Bwana Tolu yule mwanamke mimi simwamini hata kidogo. Tena nisamehe sana kwa kumtajia jina lako kwa kimbelembele changu. Hawezi kumjua jina Sudesdi na kwamba ni Mgiriki, nakataa.”
Nilimwambia mimi mwenyewe nilishangaa yeye kulitaja jina langu wakati mimi sijaonesha kwamba namjua yule mwanamke. Lakini kwa sababu aliomba msamaha nikaachana na hilo. Nikamuuliza:
“Sasa kwa nini umesema hujamuamini, wewe unajua nini?”
“Mimi najua wale wanawake si wanadamu. Ila wamejifanya wanadamu. Wanajua zaidi ya yale waliyoyasema pale.”
Nilianza kuogopa sasa. Akilini nilijiambia mwenyewe kwamba, kama si wanadamu ina maana ni majini. Na kama ni majini ina maana wanaweza kunifuata popote pale.
Tulitembea kwa haraka kwenda kwenye maduka mengine ya mbele. Tulipita duka moja la mwisho ili kuingia mtaa wa pili, nikasikia nasalimiwa:
“’Hai’ Tolu.”
Sikutaka kugeuka kwani sauti ilikuwa dhahiri kwamba ni Bi. Sheila maana ni ndogo sana.
“Si unaona bwana Tolu, sasa nahisi ni vita,” alisema Nurdin.

Tulichoona tuliamua kurudi melini ili kujinusuru na balaa lile. Tukaingia mtaa wa pili na kushika njia ya kurudi bandarini. Kufika mtaa wa mwisho, tukiwa tunapita kwenye duka la kubadilishia fedha, tukasikia sauti nyingine ya mwanamke ikisema:
“Nurdini mambo?”
Hapo ilibidi tukimbie kabisa. Tulikimbia mpaka bandarini, tukaingia kwenye meli. Kule tuliwakuta wenzetu wengine wote wamesharudi ambapo nao walitusimulia kukumbana na maajabu kama yetu.
Tulishangaa sana, mimi nilishangaa zaidi uwezo wa wale wanawake. Nilisema moyoni kwamba, endapo wameweza kujua hata mitaa tunayotoka kwenye nchi zetu basi kumbe ni waelewa wa kiwango cha juu sana.
Nahodha wetu, alicheka sana. Akasema anaamini hajuani na mtu yeyote kwenye nchi hiyo na kwamba sisi huenda tulikutana na majini ambayo yapo baharini hata wakati huo licha ya kuwakimbia kule mjini.
Tulikaa ndani ya meli kusubiri muda wa kuondoka. Lakini mimi sikutoka nje. Muda mwingi nilikuwa naangalia maji kupitia kwenye madirisha ya ndani.

Meli ilipoanza kuondoka, nilimwita Nurdin na kumuuliza kama wale akina Bi. Sheila hawawezi kutuingilia melini tukiwa majini, akasema ni suala la kumwomba Mungu wasitokee.
Nilimlaumu kimoyomoyo kwamba, alichotakiwa kuniambia Nurdin ni kwamba, hawawezi kuja kuliko kuniambia ni suala la kumwomba Mungu. Ina maana alinipa hofu badala ya matumaini.
Hali ndani ya meli ilikuwa ya utulivu wa hali ya juu kwani hakuna mtu aliyekuwa mchangamfu. Mimi nilijiuliza mengi. Nilijiuliza kama nayaona yale nikiwa nimeshapelekwa kwa mtaalam kule Sumatra je, ningekuwa sijapelekwa? Niliogopa sana.

Lakini pia nilijiuliza kwamba kama kweli wale ni majini na ndivyo ilivyokuwa kwamba ni majini na walikuja mpaka mjini. Je, sasa tukiwa baharini kwenye maji tukisafiri?
“Nurdin mimi naogopa sana. Yule mganga si alinitengeneza sasa nini tena?” nilimuuliza.
“Ondoa woga wewe. Watakuwa wanatutokea vilevile lakini hawana ubavu wa kutufanya lolote lile,” alisema Nurdin.
Ghafla nilifikicha macho kwani kama niliona kitu mbele yangu.
“Vipi tena?” aliniuliza Nurdin baada ya kuniona nimetumbulia macho mahali.
“Kama nimemwona.”
“Nani?”
“Bi. Sheila.”
Na yeye aliangalia kule nilikoangalia mimi.
“Ni wasiwasi tu hakuna lolote bwana Tolu.”

Je, nini kitaendelea? Usikose kusoma mkasa huu kwenye Gazeti la Amani, Alhamisi ijayo.

Leave a Comment