×

Kwa nini mimi tu niteswe na mapenzi kila siku?

Ni kwa upendo wa hali ya juu usiopimika, Mungu ametujalia pumzi hii inayotuwezesha kukutana tena hapa jamvini, sifa na utukufu ni kwake yeye atupaye uhai na mkate wetu wa kila siku.

Wiki hii kwenye XXLove nitazungumza na waliokata tamaa kutokana na maumivu yatokanayo na mapenzi. Walioumizwa na kuona kama kuumizwa huko ni kwao tu na si kwa watu wengine na wakati mwingine kuhisi labda maumivu ya mapenzi yameumbwa kwa ajili yao tu.

La hasha! Maumivu hayo hayako na wala hayakuumbwa kwa ajili yako. Yapo kwa kila mtu, mwanamke na mwanaume, msomi na asiyesoma, tajiri na maskini, wa kijijini na hata wa mjini, ila kila mtu ana namna yake ya kuumia na kupokea maumivu hayo.

Pole sana! Uliyeumizwa na kuteswa na mapenzi. Huna sababu ya kukata tamaa na kujiona mwenye mkosi katika maisha yako ya uhusiano, hapana, yawezekana maumivu uliyoyapata au unayoyapata wewe ni madogo kuliko yale aliyoyapata au anayoyapata jirani, rafiki, ndugu au mfanyakazi mwenzio ila anavumilia kwa sababu ni sehemu ya maisha na yanapaswa yatokee.

Kikubwa ni kufunga na kumuomba Mola akupe uwezo wa kipekee wa kumtambua mwanaume au mwanamke mwenye mapenzi na upendo wa dhati, hofu ya Mungu na aliye tayari kuishi na wewe kama mke na mume, katika shida na raha.

Usihuzunike kwa wewe kuachwa kila kukicha, tambua kuwa maumivu ya mapenzi au kitu chochote kile unachokipata katika maisha yako ya kila siku ni sehemu ya vitu vinavyoifanya dunia ijizungushe kwenye mhimili wake.

Ni lazima uyapate ili maisha yasonge mbele kwani wakati mwingine maumivu hayo yanakufanya unakuwa imara, jasiri na wakati mwingine yanakufanya unapata njia sahihi ya maisha yako.

Yanakufanya kuwa mwalimu wa wengine katika kuwafundisha namna ya kukabiliana na masaibu ya mapenzi.

Hebu maumivu hayo yachukue kama changamoto. Kama umeumizwa kwa kuachwa, kuzalishwa, kukimbiwa, kutelekezwa na kadhalika, basi kaa chini na uyakubali maumivu hayo kisha acha maisha mengine yaendelee.
Mpenzi msomaji usikose sehemu ya pili ya mada hii wiki ijayo.

Kwa maoni na ushauri, tembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mitandao wa Kijamii ya Facebook, Instagram:@mimi_na_ uhusiano au unaweza kujiunga kwenye group letu la WhatsApp kwa namba hiyo hapo juu.

Leave a Comment