×

Madhara ya kupata mpenzi wa kulipa kisasi

landscape-1452256934-mcdgrga-ec168-h

NI Jumanne nyingine yenye neema ya Mungu. Kwa neema yake tunaishi,  kwa neema yake tupo na afya. Ni jambo la kumshukuru sana Mungu kwani wale ambao hawana afya leo siyo kwamba ni watenda mabaya kuliko sisi wenye afya, ni neema tu.
Mada yangu ya leo ni madhara yanayowapata baadhi ya watu wanaoamua kupata wapenzi kwa sababu ya kulipa kisasi baada ya kuachwa au kumwagwa na wapenzi wao wa awali.

NINI MAANA YANGU?
Hapa nina maana kwamba, utakuta mtu ameachwa na mpenzi wake kwa kisa chochote kile, ila kaachwa, sasa ili aoneshe kuwa ‘bado wamo’ na kwamba hababaishwi na kuachwa huko, anaamua kuwa na mtu mwingine yeyote ilimradi tu watu waseme kaachwa na fulani lakini sasa yuko na fulani.

Hii ni mbaya sana, kwani unakuwa unampata mpenzi wa kulipizia kisasi ambaye humjui na wala hujui utafika naye wapi katika uhusiano wenu mpya.

KISA CHA KUANDIKA HIVI
Wiki iliyopita, nilikutana na kaka mmoja, akasema anaitwa Nchimbi. Nchimbi ni mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam. Anasema kuwa, alikuwa katika uhusiano wa miaka mitatu na msichana anayeitwa Nancy, lakini Machi mwaka huu, aliachwa.

“Nilichunguza sana kwa nini aliniacha, nikabaini kuwa ana jamaa mwingine ni MC kwenye shughuli za harusi, send off na hata misiba.
“Sasa ili kumwonesha kwamba  mimi bado ni kijana ninayeweza kumpata msichana yeyote, nikatafuta demu mmoja anaitwa Mage. Nadhani ni ndani ya wiki moja tu baada ya kuachwa na Nancy.

“Sasa huyo Mage bwana, hata wiki haijaisha, nikamfumania baa amekumbatiana na mwanaume, tena mzee, wamelewa chakari. Aliniomba msamaha kwamba ni pombe, nikamsamehe.

“Siku mbili mbele, simu yake iliita, nikapokea, aliyepiga ni mwanaume akanitukana sana kwamba nimepokea simu ya demu wake. Nikakata simu, nikaingia kwenye meseji, mama yangu!
“Nilikuta meseji za mapenzi karibu kumi lakini za wanaume tofauti watatu, kuna Tony, Hemed na Kulwa. Kwa kweli nikanyoosha mikono, nikamuacha,” anasema Nchimbi kwa sauti ya majuto ni mjukuu.

Anakiri kwamba, hakuwahi kupata nafasi ya kumchunguza Mage licha ya kwamba ni mkazi wa maeneo anayoishi yeye. Pia Nchimbi anasema kuwa, hakuwahi kumuuliza hata rafiki yake mmoja kuhusu Mage lakini yalipomkuta wengi wakasema walishangaa kumwona yupo na Mage.

MADHARA YAKE
Alichosema Nchimbi ni kweli kabisa, makubwa aliyokutana nayo yalitokana na kitendo cha kutaka kuwa na mpenzi wa kulipa kisasi, kwamba demu wake kabebwa na MC na yeye anataka kujitutumua kwamba bado yumo, hababaiki, matokeo yake ni kukumbana na nusu kahaba kama huyo Mage!

ELIMU YANGU
Kwa elimu yangu ya maisha ya mapenzi, inapotokea umeachwa, tulia kwanza. Tuliza akili yako na kuwa na subira ili uje upate yule atakayekuwa sahihi kwa maana ya kumchunguza kwa undani.
Unaweza kuachwa lakini ukiwa bado haujaachwa, kuna uliokuwa unawakodolea, wanakukodolea macho ila uaminifu ukawa unakuzuia, sasa wale wapitie kichwani kwa lada zako mmoja baada ya mwingine ili kumjua mwenye tabia njema na asiyekuwa na dalili ya kukuumiza baadaye.

Hii itakusaidia kuingia kwenye uhusiano imara na pengine ndoa kuliko kukurupuka kwa sababu ya kulipa kisasi. Wengi waliolipa kisasi walijikuta wamebugi na kutumbukia kwenye shimo ambalo madhara yake yameweza hata kuwasababishia vifo au kuvuruga maisha kwa jumla ndiyo maana wahenga walisema mapenzi yanaua!

TUMIA MIEZI MITANO
Miezi mitano ni mingi lakini ukiweza kuifikisha kwa kukaa mwenyewe kabla ya kuingia kwenye uhusiano mpya, itakusaidia kumpata aliye halisi. Wengine wakiachwa leo Jumanne keshokutwa Alhamisi tayari ana  mwingine, eti ‘kata mti panda mti’ ndiyo itasaidia kuondoa maumivu na kumsahau wa awali, nani kasema!

KUNUNUA NA KUSOMA MAGAZETI YA GLOBAL PUBLISHERS ONLINE, INGIA HAPA==>VODACOM M-PAPER APP

*********

JIUNGE NA SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

ERIC SHIGONGO INSTAGRAM: @ericshigongo

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

Leave a Comment