×

Mapenzi ni sehemu ya maisha, kwa nini tunawabania wanafunzi?

students.jpgHivi karibuni nilikutana na vijana wanaosoma katika shule moja ya sekondani iliyopo Lushoto mkoani Tanga iitwayo Mlalo Sekondari. Wanafunzi hao walikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujifunza kutoka kwangu mbinu wanazoweza kuzitumia ili wafaulu katika mitihani yao.

Nilizungumza nao mambo mengi lakini mjadala mkubwa ulikuwa pale nilipotaja suala la mapenzi kama moja ya sababu ambayo imekuwa ikiwafanya wanafunzi wengi kufeli katika mitihani yao.

Bila woga wala aibu, kuna wawili walieleza jinsi ambavyo wanayachukulia mapenzi kama sehemu muhimu ya mwanadamu yeyote aliye na akili timamu. Wakasema, eti ni vigumu sana kujiweka mbali nayo kutokana na mfumo wa sasa wa maisha.

Nilitumia ufahamu wangu kuwaeleza madhara ya kuchanganya mapenzi na elimu, mwisho wa siku nikaona kama wamenielewa. Hapo ndipo nikajiwa na wazo la kuandika makala haya nikiamini wanafunzi watakaopata nafasi ya kuisoma wanaweza kupata elimu, lakini pia wazazi wakisoma watatumia nafasi yao kuwaelimisha watoto wao katika hilo.

Mpenzi msomaji wangu, kama kuna asiyefahamu maana ya mapenzi basi kuanzia leo ajue kuwa mapenzi ni ulevi kama vilevi vingine. Mtu anayependa hulewa na ulevi wake ukimkolea hujikuta anaharibu ufahamu wake kama mtu aliyelewa pombe.

Walevi wa mapenzi huweza kufanya mapenzi hata barabarani sehemu ya wazi, huku akili zao zikiwapa taarifa kwamba watu hawawaoni. Mambo ya aina hii hufanywa pia na walevi wa pombe.

Lakini ulevi wa mapenzi una nguvu kubwa ya kuiteka akili na kumtia mtu mshawasha kiasi cha kuacha kazi muhimu na kukimbilia kufanya ngono.

Hivyo, mwanafunzi ambaye anataka mafanikio ya kimasomo lazima aweke kando masuala ya mapenzi kwa lengo la kutoitwika akili mzigo ambao kwa umri wa wanafunzi wengi, hasa wa kike ambao ni waitikiaji wa kauli za wavulana ni vigumu kwao kuhimili.

Licha ya baadhi ya wataalam wa masuala ya afya kubainisha faida za kufanya mapenzi kwa afya ya mwili, bado uchunguzi unaonesha kuwa wanafunzi wengi ambao wengi wao huwa katika umri mdogo, hushindwa kuzuia hisia za mapenzi na kujikuta wanakuwa watumwa wa ngono.

Mapenzi kwa mwanafunzi yana hasara za aina mbili. Kwanza, mapenzi yanapokuwa moto huteka hisia na kumfanya msomi atumie muda mwingi kuwaza juu ya mahaba na hivyo kuufanya ubongo uone kuwa mapenzi ni kitu muhimu na hivyo kujituma kuhifadhi mambo ya mapenzi kuliko masomo.

Jambo la pili ni machungu ya mapenzi hasa unapotokea mfarakano. Kwa mfano kuachwa, kusalitiwa, kuudhiwa, kugombana na migogoro yote ya kimapenzi huleta msongo wa mawazo na kumfanya mwanafunzi asiweze kusoma kwa kiwango stahili. Hivyo, inashauriwa kuwa mwanafunzi asijihusishe kabisa na mapenzi.

Ndiyo! Mapenzi yakae pembeni kwanza, yatafuta baadaye. Sasa hivi kila aliye shuleni ajue mapenzi ni adui mkubwa wa mafaniko yake, hivyo ayape kisogo, aelekeze akili yake kwenye kusoma kisha baadaye akiwa ameshafaulu na kuwa na kazi yake, mapenzi yatajileta yenyewe.

Wapo wanaosema, mbona f’lani ana mpenzi na bado anafanya vizuri shuleni. Niseme tu kwamba, kila mtu ana akili na bahati yake. Yawezekana huyo unayemuona anaendekeza mapenzi na bado anafaulu kwenye mitihani huenda ni kibahatibahati tu.

Sasa kwa wewe ambaye una ‘kichwa cha panzi’ halafu unataka kuchanganya mapenzi na elimu eti kisa shosti wako mwenye wapenzi kibao anafanya vizuri, ipo siku utajuta!

Leave a Comment