×

Jinsi uzito unavyoathiri uzazi kwa mwanamke

pregnant-black-womanTunapozungumzia uzito unavyoathiri uzazi kwa mwanamke, hapa tunamaanisha uzito uwe mkubwa au mdogo vyote vina madhara makubwa katika uzazi.

Madhara haya yanayotokana na uzazi ni mwanamke kutopata ujauzito au kutozaa. Hali hii ya kutozaa au kutopata mimba tunaita ugumba.

Mwanamke atahesabika kwamba ni mgumba endapo atatafuta mtoto kwa muda usiopungua mwaka mmoja na asifanikiwe huku tendo la ndoa au kujamiiana likifanyika kikamilifu siku za kupata mimba.

Siku za kupata mimba tutazizungumzia kwa undani katika makala zijazo ila kwa ufupi ni vema mwanamke afahamu vizuri mzunguko wake wa hedhi.

Mzunguko wa hedhi unaanza kuhesabu siku ya kwanza ni ile uliyoona damu ya hedhi na mwisho wa mzunguko ni siku moja kabla hujaona kwa mwezi unaofuata, hapa haijalishi zile siku za damu.

Mzunguko wa hedhi upo mfupi ambao ni siku 22 hadi 27, wa kawaida ni siku 28 hadi 30, na mrefu ni siku 31 hadi 35. Mzunguko wa hedhi uwe mrefu, mfupi au wa kawaida umegawanyika katika makundi mawili, kwanza ni ule unaopevusha mayai na pili ni ule usiopevusha mayai.

Mwanamke mwenye mzunguko unaopevusha mayai ndiye anayepata mimba. Dalili za upevushaji mayai ni  kupata ute wa uzazi. Ute wa uzazi upo wa aina tatu; kwanza ni mwepesi, pili ni ule unaovutika na tatu mzito.

Ute unaovutika ndiyo unaoashiria yai limetoka na mimba ipo tayari kutungwa. Katika kipindi hiki cha upevushaji mwanamke hupata dalili nyingine mbali ya ute wa uzazi ambazo tutakuja kuona katika makala zijazo.

Mwanamke mwenye mzunguko usiopevusha mayai hapati au haoni ute wa uzazi hivyo hapati ujauzito ingawa atakuwa anapata damu ya hedhi kama kawaida. Mwanamke huyu wakati mwingine hupata ute nzito daima ukeni ambao hauna harufu wala muwasho. Endapo mwanamke atapata ute mzito ukeni wenye muwasho na harufu, basi amuone daktari wa akina mama afanyiwe vipimo ili kujua tatizo ni nini. Kama hutafanyiwa uchunguzi makini, ndipo hapo sasa tatizo linakuwa linajirudia mara kwa mara ambapo utamsikia mwanamke akilalamika, kila akitibiwa tatizo linajirudia na amehangaika sana bila mafanikio.

ATHARI ZA UZITO MKUBWA

Mwanamke mnene huonekana kwa macho, huwa na mrundikano wa mafuta tumboni, mabegani, kifuani, usoni hasa mashavu, shingo na makalio pamoja na mapaja. Hulalamika nguo nyingi kumbana na daima huwa na hamu ya kula na hata kujihisi mwili unakuwa mzito.

Vifuko vya uzalishaji wa mayai ya uzazi kwa mwanamke hutegemea zaidi uzito wa mwili wa mwanamke, endapo mwanamke atakuwa mwembamba sana atapata hali iitwayo kitaalamu Hypothalamic Hypogonadism. Kwa hiyo mwanamke mwenye mafuta mengi tumboni, au tumbo kubwa au kitambi hupata tatizo liitwalo kitaalamu Insulin Resistant na husababisha vifuko vya mayai kushindwa kuzalisha mayai au kufanya kazi zake za kuzalisha vichocheo vya uzazi na kusababisha kutokea vivimbe kwenye vifuko vya mayai na hivyo mwanamke anapata ugonjwa uitwao PCOS, au Polycystic Ovarian Syndrome.

Itaendelea wiki ijayo.

Leave a Comment