
Wiki hii kwenye safu hii tunaye msanii wa filamu, Rammy Galis ambaye anajibu maswali 10 aliyoulizwa na Mwandishi Wetu Boniface Ngumije.
Ijumaa: Wengi wangependa kujua safari yako ya kisanii ilianzia wapi!
Galis: Ilianza mwaka 2012 baada ya kukutana na marehemu Steven Kanumba.
Ijumaa: Kabla ya kujiingiza kwenye filamu ulikuwa unajishughulisha na nini?
Galis: Nilikuwa nafanya kazi ya uhasibu katika Sekta ya Magari Bandari Kavu Veta.
Ijumaa: Kipi ambacho unajivunia kutoka kwa Kanumba?
Galis: Alifufua ndoto zangu, lakini pia nimejifunza kutoka kwake kuwa kila kitu kinafanikiwa pale mtu anapokuwa na juhudi.
Ijumaa: Wanakuita pacha wa Kanumba, hivi viatu ‘Santana’ vyake vinaweza kukutosha kweli?
Galis: Kwa hilo sina wasiwasi kutokana na ubora wa kazi zangu.
Ijumaa: Vipi kuhusu kazi uliyofanya hivi karibuni Nigeria na ilikuaje mpaka ukapata shavu?
Galis: Mwaka jana nilisafiri na kazi zangu mpaka Acra, Ghana kutafuta wasanii wa kufanya nao kazi. Nilikwenda kule sifahamiani na mtu yeyote yule na nilifikia kwenye shirikisho la filamu la huko na kuwaonesha kazi zangu nikiomba wanisaidie niweze kufanya nao kazi.
Baada ya kuowanesha waliniambia tatizo linalofanya sisi tusitusue ni lugha. Lakini mmoja wa wafanyakazi wa shirikisho hilo alipenda muonekano na kazi zangu, akaniunganisha na direkta mmoja wa Ghana ambaye wakati huo alikuwa Nigeria. Huyo tulifanya mawasiliano nikamuonesha pia kazi zangu akazikubali ndipo tukapanga kufanya filamu ya Red Flag tuliyoianzia hapa nyumbani na kuimalizia Lagos, Nigeria.
Ijumaa: Baada ya kufika Nigeria kuna ‘mashavu’ mengine uliyopata?
Galis: Yap, Wanigeria walionekana kunikubali sana na nikafanya nao baadhi ya filamu.
Ijumaa: Kuna tofauti gani kati ya wasanii wa Bongo na nje mnapokuwa location?
Galis: Usiriasi katika kazi. Wenzetu wanajali sana wanachofanya kuliko sisi.
Ijumaa: Unafikiri nini hasa changamoto zinazoikumba tasnia ya filamu Bongo?
Galis: Wasanii hatuna uhakika wa kuuza kazi zetu. Lakini pia uhalali wa kuzimiliki haupo. Hizo ni changamoto kubwa kwetu.
Ijumaa: Ukiachana na kazi kuna tetesi kuwa unapika na kupakua na Agnes Masogange, ukweli upo vipi?
Galis: Dah! Hata kama kuna ukweli siko tayari kuweka wazi kila kitu kwa sasa, ila Agness ni mtu wangu wa karibu.
Ijumaa: Jambo la mwisho ambalo unaweza kuwaachia mashabiki wako.
Galis: Waniamini, sasa nimekuwa wa kimataifa. Safari yangu ya Nigeria imenikutanisha na waigizaji wakubwa ambao wamenifanya nizidi kuwa bora.