The House of Favourite Newspapers

Mayanja mguu ndani, mguu nje Simba SC

0

mayanja

Jackson Mayanja.

Hans Mloli, Dar es Salaam
HARAKATI za Simba kutafuta kocha mkuu mpya zimezua mapya baada ya kuibuka kitendawili juu ya kibarua cha kocha msaidizi wa timu hiyo, Mganda, Jackson Mayanja kama ataendelea kuwa na kikosi hicho msimu ujao.
Hiyo imekuja baada ya kauli iliyotolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe iliyomaanisha kuwa hatma ya Mayanja sasa itakuwa mikononi mwa kocha huyo mpya ambaye hajajulikana ni nani mpaka sasa japokuwa kuna listi ndefu ya wanaotajwa kuhitajika.
Katika mahojiano aliyoyafanya Hans Poppe hivi karibuni jijini Dar alikaririwa akisema kuwa bado wanaendelea kutafuta kocha mpya na ndiye atakayeamua kuhusiana na msaidizi wake maana itategemea na mapendekezo ya bosi huyo mpya wa benchi la ufundi maana wengine hupenda kuja na wasaidizi wao.
“Kocha mkuu mpya anakuja, hatujajua kuhusu mapendekezo yake, haijajulikana sasa, kwamba baada ya kutua kocha mpya atakuja na mapendekezo gani, abaki naye aendelee kufanya naye kazi au kama atakuja na  msaidizi wake, haijajulikana bado,” alisema Poppe.
Championi Jumatano lilimtafuta Mayanja aliye kwao Uganda kuzungumzia suala hilo, alisema: “Ninachofahamu ni kwamba mkataba wangu umekwisha na nilishazungumza na uongozi na wakaniambia naweza kuendelea nao msimu ujao katika cheo changu cha kocha msaidizi, kwa hiyo yaliyobaki mengine nawasikilizia wao.”
Mayanja alitua Simba katikati ya msimu uliopita kama kocha msaidizi anayekaimu nafasi ya kocha mkuu aliyetimuliwa kikosini hapo, Muingereza, Dylan Kerr.

Leave A Reply