Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mh. Amina Masenza.
Stori: Godwin, Risasi Jumamosi, Iringa
MKOA wa Iringa umeonesha kushamiri kwa haraka kama mabasi ya mwendokasi kwa kubainika watumishi hewa waliongezeka kutoka watumishi 27 wa awali walioripotiwa kwa Rais Dk. John Magufuli hadi kufikia watumishi 169.
Idadi hiyo ya watumishi hewa walioibuliwa ndani ya muda mfupi, imedaiwa kugharimu mishahara hewa ya takriban shilingi milioni 364,028,910.80 wakiwemo watumishi ambao ni marehemu waliolipwa shilingi milioni 53.
Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ambayo awali katika taarifa aliyopelekewa Rais ilionesha hakuna mtumishi hewa, sasa wamenaswa watumishi hewa 67 waliotafuna fedha za umma takriban shilingi milioni 226,665,510.50.
Huku watumishi hewa wawili kutoka Wilaya ya Mufindi na Kilolo waliokuwa wakitumia cheti cha mtumishi aliyeajiriwa Hospitali Teule ya Iringa (Hospitali ya Ipamba) wamedaiwa kutoweka kusikojulikana katika mazingira ya kutatanisha kufuatia msako wa watumishi hewa unaoendelea mkoani Iringa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amewaambia waandishi wa habari kuwa anaendelea kuwasaka watumishi waliohusika na kusababisha tatizo hilo kila kona ya idara za halmashauri za mkoa wa Iringa ambapo baadhi wameanza kurejesha fedha walizochukua lakini suala la kuwachukulia hatua za kisheria amesema lipo palepale.
“Aprili 18 nilitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya hali ya uwepo wa watumishi hewa katika Mkoa wa Iringa, nilieleza kuwa ili kujiridhisha na kuondolewa kabisa kwa watumishi hewa katika Mkoa wa Iringa nitaunda timu ya wataalam kwa ajili ya kupita katika hospitali teule zote za wilaya na kwenye mamlaka za serikali za mitaa kwa lengo la kuendelea kubaini iwapo wapo watumishi hewa ambao hawakubainishwa katika zoezi la awali.
“Aidha, niliahidi kutoa taarifa kwenu mara zoezi hilo litakapokamilika. Timu niliyounda imekamilisha kazi yake Juni 7, mwaka huu na kunikabidhi taarifa yake,” alisema Amina.
Mkuu huyo wa mkoa alisema ulipaji wa mishahara isivyostahili umeisababishia serikali hasara ya shilingi milioni 364,028,910.80 katika Mkoa wa Iringa.
Alisema timu hiyo pia imebaini katika Hospitali Teule ya Ilula inayotoa huduma Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo lipo tatizo la fedha za mishahara isiyolipwa inayofikia shilingi milioni 151,583,969.00 kutorejeshwa hazina tangu Januari, 2008 hadi Februari, 2016.
Hata hivyo, alisema shilingi milioni 53,825,362.75 ni fedha hewa ambazo zimelipwa kwa watumishi waliofariki dunia wakati wastaafu wamelipwa mishahara hewa shilingi milioni 83,538,037.55 na watoro na waliofukuzwa kazi wamelipwa shilingi milioni 226,665,510.50 na kufanya jumla ya mishahara hewa kufikia shilingi milioni 364,028,910.80
“Mkoa unaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa katika taarifa ya tume na ninaahidi kuendelea kutoa taarifa ya utekelezaji baada ya kuyafanyia kazi,” alisema.