MSANII kutoka Rocky City, aliyejulikana zaidi kwa Wimbo wa Iveta, Faraji Twaha ‘Sajna’ hivi karibuni amefungukia ukimya wake kwenye gemu kuwa ulisababishwa na kupotezwa na aliyekuwa bosi wake ambaye pia alikuwa anamiliki Studio ya Tetemesha Records, Kidbway.
Akichonga na gazeti hili, Sajna alisema Kidbway aliamua kuacha kufanya naye kazi baada ya yeye kutokuwa na maelewano mazuri na menejimenti yake jambo ambalo analichukulia ni sawa na kumuacha apotee maana bado jina lake lilikuwa dogo lakini pia hata kiumri hakuwa na uwezo wa kupambana na changamoto za gemu akiwa mwenyewe .
“Kiukweli baada ya Kid kuniacha nilipoteza kabisa ramani kimuziki maana kila ngoma niliyokuwa nafanya katika studio zingine hazikuwa zikisikika, lakini kwa sasa ninajipanga kivingine na nimefanya kazi nne ambazo hazijatoka ambazo ni Yaleyale, Tahani, Kisura pamoja na Karoge,” alisema Sajna na kumaliza kuwa anahitaji sapoti kutoka kwa wapenzi na wadau wa muziki ili aweze kupeperusha vyema bendera ya jiji la miamba.
