NI Jumanne nzuri yenye utulivu nikiamini kuwa, Mungu ametupa upendeleo wa aina yake mpaka kufikia uhai tulionao. Siku zote nasema, si kwa sababu ya nguvu zetu wala maarifa, bali ni neema yake tu.
UJUMBE KWENU WANAWAKE
Ujumbe wangu wa leo kwa shoga zangu ni kuhusu mambo yetu ya ndoa. Si mnajua tena mambo ya chumbani zaidi?!
Shoga, kuna tabia naijua ipo lakini si nzuri kwani inadhalilisha sana. Wapo wanawake tena wapo kwenye ndoa zao lakini mambo wanayoyafanya wakiwa chumbani na waume zao ni aibu!
MUACHE MAKUSUDI
Utakuta mwanamke anajua kabisa chumba chake kimepakana na chumba cha watoto au pengine na chumba cha majirani, kiasi kwamba hata akiimba nyimbo zake za taarab, chumba cha pili wanasikia vizuri tu, lakini wao wakiwa kwenye ‘makasheshe’ hawajali hilo ni kelele mtindo mmoja.
Hii tabia nailaani kupita kiasi kwani ni kujidhalilisha sana. Unapoonesha mzuka chumbani kwako mpaka chumba cha pili wanasikia, unawapa ujumbe gani wao, kwamba wao hawawezi au wewe ndiyo unajua kuponda raha za mahaba?
KUPAGAWA HUKU NOMA
Mbaya zaidi, wanawake wengine mzuka ukipanda wanapiga kelele huku wanasema kila kitu kinachoendelea! Jamani, ustaarabu wa wapi huu? Yaani wewe uzuzuke na mumeo chumbani, useme kila kitu halafu chumba kinachofuata, mtoto wako anasikia kwamba mama yuko vipi? Mbaya!
MADHARA YA MZUKA WAKO
Tabia kama hii, maeneo mengi sana ndiyo imezalisha watoto makahaba, imezalisha mimba za utotoni, imezalisha watoto wasio na staa kwa sababu hakuna kitu mtoto asichokijua na mbaya zaidi amekijua kupitia kelele za mama yake.
We unadhani mtoto wako siku ya kwanza kusikia hizo kelele zako kama alikuwa hajui ni za nini si atawauliza watoto waliomzidi umri, sasa wao ndiyo watammwagia kila kitu, kwamba ukisikia hivyo ujue mama yako amepandisha mzuka! Amepandishaje? Watamwambia kapagawa! Kapagawaje? watamwambia! Loo!
WITO WANGU
Wito wangu kwenu ni kwamba, kila mtu anajijua tabia yake. Wapo ambao wakiwa ‘kazini’ wao ni kununa mwanzo mwisho, wengine wao ni kukodoa macho tu, wengine mbwembwe nyingi lakini vitendo hakuna, wengine ni kelele kama wako kwenye mkutano wa siasa, kwa hiyo vizuri kusoma mazingira.
Unapohamia kwenye nyumba nyingine, angalia chumba cha watoto kiwe wapi, chumba chako kiwe wapi! Kama kuna majirani, angalia wao chumba kipo wapi, stoo iko wapi!
EPUKA KUWA KITUKO
Siyo unaingia tu, unasema chumba chetu hiki halafu usiku unakuwa kituko, matokeo yake asubuhi unapotoka kwenda dukani kununua mkate, unashangaa kuwaona majirani wanakuchungulia kwa sababu ya sinema yako ya bure ya jana usiku.
Mzuka haukataliwi, tena ni mzuri sana kwa sababu unaongeza chachandu ya usiku lakini je, chumba chako kinapakana na nani!?
Kama hakuna jinsi, maana vyumba vingine vimebana kotekote, basi huna budi kupandishia mzuka ndani kwa ndani na wala usijidanganye kufungulia redio kwa sauti ya juu eti hawatakusikia, kwani sauti ya redio na sauti ya mzuka vitu viwili tofauti.
Tuonane wiki ijayo jamani.