ASAALAM aleykum wapendwa wasomaji wa safu hii. Hongera sana kwa wale wenzetu wanaokwenda sawa na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kwa maana angalau wanatufanya na sisi kujutia nafsi zetu, mana’ke mambo mengine tunayofanya tunayajua wenyewe.
Vipi, kwani yale madongo niliwatupia wiki jana yaliwaingia sana? Maana nimeona watu povu limewatoka, kila ninapopita mashosti wananirushia lawama, lakini nitafanyaje sasa wakati nyie wenyewe ndiyo mnataka niwape uzoefu?
Basi baada ya kumaliza ishu yetu ya wiki iliyopita, leo acha nikupe kitu kingine ambacho kitakupa somo, kama nilivyokueleza kuwa rafiki yako aishie hukohuko, asimsogelee mumeo, maana ushosti wa siku hizi ni kama mshumaa, unamuonesha mwanga mwenzako huku mwenyewe unateketea.
Ninawalenga wale wenzangu na mimi, ambao Mwenyezi Mungu amewajaalia, alhamdulilah maisha yapo na kwa hiyo, wanaishi na wadada wa kazi ambao tunawaita mahausigeli. Wakishafikia hatua hiyo, hujiona wao ndo wao, wamekuwa matajiri, mambo yao yamenyooka.
Basi kutwa kumfanyisha kazi mtoto wa mwanamke mwenzake utafikiri mashine. Mara amtume hiki, mara kile, yaani kama umemtembelea hadi unaona uchungu. Basi umfanyishe kazi namna hiyo, mwoneshe angalau utu basi, bado masimango juu.
Tena wanasubiri wakati wa chakula, mara utawasikia, kwenu ulikuwa unakunywa chai ya maziwa, nyama mlikuwa mnasubiri sikukuu, mara sijui nini na nini, yaani hadi mtu unaangua machozi na kujiuliza, hivi huyu angekuwa binti yangu, ndiyo anafanyiwa hivi!
Afadhali basi ufanye yote hayo, halafu umlipe kulingana na kazi anazofanya, lakini vyote hivyo, mwisho wa mwezi mtu anapata mshahara wa elfu 25, jamani, hivi hela hiyo mtu utafanyia kitu gani? Maana bora unyanyasike, lakini mshahara uwe afadhali, unajua angalau utaweza kuwekeza kidogokidogo upate kamtaji uachane na masimango.
Unafanya hivyo, huku ukijua kuwa huyo ndiye anakupikia chakula wewe na familia yako, ndiye anakulelea watoto wako na ndiye mlinzi mkuu wa nyumba na mali zote zilizomo ndani.
Shosti, nikuambie leo, kama kuna wadudu wabaya ambao hupaswi kuwachokonoa, basi ni hawa wadada wasaidizi wa kazi. Kwanza ni hatari kwa ndoa yako. Mdada akiona kwa mama ni moto, atajisogeza kwa baba na kuanza kumrembulia macho.
Wazungu wanasema body language, anamuonesha baba kuwa yupo tayari kwa lolote na kama mnavyojua wanaume wenyewe hawa, shauri yako.
Lakini pia kwa usalama wako mwenyewe na familia yako, hujasikia watu wa familia wakifa kwa sumu, nyumba kuchomwa moto au mali kubwa kuibwa? Hawa wanaamua kukomoa na kulipa kisasi. Jichunge sana shosti, usijesema Shangingi Mstaafu sikukutosha!