×

Usiku wa Sikinde, Msondo hapatoshi Dar Live

sikinde

PATAKUWA hapatoshi! Unaweza sema hivyo kwa maana nyingine baada ya Bendi ya Mlimani Park Ochestra, au wana Sikinde Ngoma ya Ukae wakiongozwa na mkali wa kuimba Rhumba, Hassan Rehani Bitchuka ‘ Super Sterio’ watakapokutana na Msondo Music Band chini ya Shaaban Dede ‘Kamchape’ katika bonge moja la shoo, Sikukuu ya Idd Mosi ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar.

Akizungumza na Risasi Jumamosi, Kiongozi wa Sikinde, Abdallah Hemba amesema usiku huo wataonesha umahiri mkubwa sambamba na kuwapa mashabiki wao wimbo unaotamba sasa wa Jinamizi la Talaka ambao upo katika albamu yao mpya iliyo na vibao vinane.

msondo ngoma music band“Nyimbo zote za zamani zitakumbukwa siku hiyo zikiwemo Kasimu wa Kustarehe, Selina, Talaka Rejea, Tui la Nazi,” anasema Hemba ambaye ni muimbaji atakayesaidiana na wapiga magitaa mahiri, Mjusi Shemboza, Steven Kaingilila Maufi, Tony Bass na mpiga tumba Ally Jamwaka huku drums zikipigwa na Habib Jeff.

Nyimbo zingine zilizovuma zamani ambazo nazo zitapigwa ‘laivu’ kwa kutumia vyombo ni Hiba, Fikiri Nisamehe, Barua Kutoka Kwa Mama, Neema na kadhalika.

Naye Kiongozi wa Msondo, Dede amesema kuwa wamejipanga vya kutosha wakiwa na wanamuziki mahiri kama vile Roman Mng’ande ‘Romario,’ Salehe Bangwe na bila kuwasahau Huruka Uvuruge na mzee mzima Said Mabera, mpiga solo mahiri ambaye tangu ajiunge katika bendi hiyo zaidi ya miaka 20 iliyopita hajathubutu ‘kuikimbia.’

“Mashabiki watarajie kutusikia kwa nyimbo kibao usiku huo kuanzia Kicheko, Mawifi Mnanionea, Ndoa Ndoana, Nimezama Katika Dimbwi, Mti Mkavu na Mizimu.

“Nyimbo nyingine zitakazotikisa siku hiyo ni pamoja na Wabakaji, Tabu, Pricila, Penzi la Mlemavu, Piga Ua Talaka Utatoa, Tuma, Wapambe, Asha Mwana Sefu, Ajali, Mtanikumbuka, Barua ya Kusikitisha, Mwana Mkiwa,  Kalunde, Kaza Moyo, Jesca, Kwenye Penzi, Binti Maringo na nyingine nyingi,” alisema Dede ambaye kwenye safu ya uimbaji atasaidiana na Juma Katundu, Hassan Moshi William ‘TX Junior’ na Hussein Kalembo.

Kiongozi wao mwingine, Saidi Mabera ataongoza safu ya wapiga magitaa ya solo na Rhythm ambao ni Ridhiwani Pangamawe na Huruka Uvuruge, Ramadhani Zahoro Bangwe na Mustafa Hamis ‘Pishuu’.

Kwa upande wa gitaa zito la besi watakuwepo Ally Lindunga na Saad Ally ‘Sure Boy’ na drums zitachanganywa na Arnold Kang’ombe.

Naye Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo alitia neno kuwa mbali na bendi hizo pia usiku huo burudani itaporomoshwa na mkali wa Mchiriku, Msaga Sumu, East African Melody na Wakali Dancers kwa kiingilio cha Sh.7,000 tu.

 

Leave a Comment