×

Ndoa ya Upendo Kilahiro yavunjika

upendo kilahiro1Upendo Kilahiro.

Musa Mateja na Imelda Mtema

Risasi Jumamosi

DAR ES SALAAM: Kuna madai kwamba, Mahakama ya Mwanzo, Manzese/Sinza jijini Dar imeridhia kuvunjika kwa ndoa ya mwimbaji maarufu wa muziki wa  Injili Tanzania, Upendo na mumewe Amon Kilahiro huku mwanaume huyo akijibu tuhuma hizo kwa gazeti hili, twende pamoja.

Habari zinadai kwamba, ndoa ya wawili hao ilivunjwa na mahakama hiyo Machi mwaka huu, mbele ya Hakimu Elias Mwamelo ambaye kwa sasa amehamishiwa mahakama nyingine.

Ili kuweka mizani ya habari hiyo, Alhamisi iliyopita, gazeti hili lilimtafuta Amon ili kumsikia anasemaje kuhusu kuwepo kwa madai hayo ambapo mahojiano yake yalikuwa hivi:

amon-kilahiro3Amon Kilahiro.

Risasi Jumamosi: Samahani sana, naongea na Amon Kilahiro?

Amon: Ndiyo, nani mwenzangu?

Risasi Jumamosi: Hapa ni Gazeti la Risasi Jumamosi. Kuna madai kwamba, ndoa yako na mkeo, Upendo imevunjika kwa maamuzi ya Mahakama ya Mwanzo, Mazenze/Sinza ni kweli?

Amon: Nani amekupa habari hizo?

Risasi Jumamosi: Ni vyanzo ambavyo hatuwezi kuviweka wazi kwako.

Amon: Je, ni sawa ukiandika habari ya mtu kwamba amekufa halafu hajafa?

Risasi Jumamosi: Ndiyo maana ya kukupigia wewe, kwamba unasemaje kuhusu madai hayo? Maana Upendo mwenyewe tumesikia yupo nchini Marekani.

Amon: Ni kweli alikuwa Marekani lakini amerudi.

Risasi Jumamosi: Hebu tupe ukweli.

Amon: Je, nikisema mimi sitaki muiandike habarii hiyo?

Risasi Jumamosi: Sababu ya kukupigia ni kutaka kuiandika ndiyo maana tumeomba ushirikiano wako.

Amon: Ngoja niwape namba ya mchungaji wangu.

Hata hivyo, Amon hakumtaja jina mchungaji wake wala hakusema ni wa kanisa la wapi, ila alimtajia namba mwandishi.

Namba hiyo aliyosema ni ya mchungaji ilipigwa, ikapokelewa, ikawa hivi:

Risasi Jumamosi: Za leo?

‘Mchungaji’: Nzuri tu.

Risasi Jumamosi: Naongea na mchungaji?

‘Mchungaji’: Hapana. Mimi si mchungaji?

Risasi Jumamosi: Wewe si mchungaji wa Amon Kilahiro, upo Dar?

‘Mchungaji’: Hapana, mimi niko Mtwara huku.

Ilibidi Risasi Jumamosi lirudi kwa Amon kwa kumpigia simu ili kumjulisha kwamba, namba aliyotupa huenda kuna makosa, lakini simu yake ikawa inaita bila kupokelewa.

Baada ya hapo, gazeti hili lilifika  kwenye mahakama hiyo iliyopo, Sinza Makaburini, Dar na kuulizia kama kulikuwa na kesi hiyo ambapo mmoja wa makarani ambaye hakupenda kutaja jina lake alisema ni kweli kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo na kusikilizwa na Hakimu Elias Mwamelo ambaye alitoa hukumu ya talaka Machi, mwaka huu.

Paparazi wetu alianza kumtafuta Upendo Kilahiro ili aweze kuthibitisha kwa mdomo wake madai hayo, lakini muda wote hakupatikana hewani, lakini habari zilisema kuwa, kwa sasa yupo Marekani.

Risasi Jumamosi likamtafuta Katibu wa Chama cha Waimba Injili Tanzania, Stella Joel kwa lengo la kutaka kujua kama taarifa hizo zipo kwenye meza yake, ambapo baada ya kupatikana alisema anazo habari hizo ingawa si rasmi kutoka kwa Upendo mwenyewe.

“Kusema kweli sisi hapa hatuna taarifa rasmi kutoka kwa Upendo, ila taarifa za kupeana talaka mahakamani tunazo, hivyo siwezi kuzungumzia zaidi ishu hii kwakuwa walengwa hawajaamua kuweka bayana kwetu, ila Upendo yupo Marekani,” alisema Stella.

Gazeti hili likamtafuta mwimba Injili, Upendo Nkone anayedaiwa ni ndugu na Amon ili kumuuliza kama anajua chochote kuhusu Upendo, alisema:

“Kuhusu nini? Mimi najua yupo Marekani.”

Risasi Jumamosi: Vipi, kuhusu ndoa yake?

Upendo: Mimi najua yupo Marekani (akakata simu).

Leave a Comment