The House of Favourite Newspapers

Dede, Bitchuka uso kwa uso Idd Mosi Dar Live

0

sikindeELVAN STAMBULI

MKONGWE wa Muziki wa Dansi kutoka Bendi ya Mlimani Park Ochestra ‘Wana Sikinde Ngoma ya Ukae’, Hassan Rehani Bitchuka ‘Super Sterio’ anatarajiwa kukutana uso kwa uso na mkongwe mwenzake kutoka Msondo Music Band, Shaban Dede ‘Kamchape’ katika bonge moja la shoo, Sikukuu ya Idd Mosi hii ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar.

Akizungumza na Over Ze Weekend, Kiongozi wa Sikinde, Abdallah Hemba amesema usiku huo wataonesha umahiri mkubwa sambamba na kuwapa mashabiki wao wimbo unaotamba sasa wa Jinamizi la Talaka ambao upo katika albamu yao mpya iliyo na vibao vinane.

msondo“Nyimbo zote za zamani zitakumbukwa Idd Mosi hii zikiwemo Kasimu wa Kustarehe, Selina, Talaka Rejea, Tui la Nazi,” anasema Hemba atakayesaidiana na wapiga magitaa mahiri, Mjusi Shemboza, Kaingilila Maufi, Tony Bass na mpiga tumba Ally Jamwaka huku drums zikipigwa na Habib Jeff.

Nyimbo zingine zilizovuma zamani ambazo nazo zitapigwa ‘laivu’ kwa kutumia vyombo ni Hiba, Fikiri Nisamehe, Barua Kutoka Kwa Mama, Neema na kadhalika.

Naye Kiongozi wa Msondo, Dede amesema kuwa wamejipanga vya kutosha wakiwa na wanamuziki mahiri kama vile Roman Mng’ande ‘Romario,’ Salehe Bangwe na bila kuwasahau Huruka Uvuruge na mzee mzima Said Mabera, mpiga solo mahiri ambaye tangu ajiunge katika bendi hiyo zaidi ya miaka 20 iliyopita hajathubutu ‘kuikimbia.’

“Mashabiki watarajie kutusikia kwa nyimbo kibao usiku huo kuanzia Kicheko, Mawifi Mnanionea, Ndoa Ndoana, Nimezama Katika Dimbwi, Mti Mkavu na Mizimu.

“Nyimbo nyingine zitakazotikisa siku hiyo ni pamoja na Wabakaji, Tabu, Pricila, Penzi la Mlemavu, Piga Ua Talaka Utatoa, Tuma, Wapambe, Asha Mwana Sefu, Ajali, Mtanikumbuka, Barua ya Kusikitisha, Mwana Mkiwa, Kalunde, Kaza Moyo, Jesca, Kwenye Penzi, Binti Maringo na nyingine nyingi,” alisema Dede ambaye kwenye safu ya uimbaji atasaidiana na Juma Katundu, Hassan Moshi William ‘TX Junior’ na Hussein Kalembo.

Kiongozi wao mwingine, Saidi Mabera ataongoza safu ya wapiga magitaa ya solo na Rhythm ambao ni Ridhiwani Pangamawe na Huruka Uvuruge, Ramadhani Zahoro Bangwe na Mustafa Hamis ‘Pishuu’.

Kwa upande wa gitaa zito la besi watakuwepo Ally Lindunga na Saad Ally ‘Sure Boy’ na drums litachanganywa na Saad Ally ‘Mashine’ na Arnold Kang’ombe.

Tarumbeta zitapulizwa na kijana machachari Roman Mng’ande na Hamis Mnyupe. Dorice George atapiga tumba, drums atazikung’uta Amiri Said Dongo.

Naye Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo alitia neno kuwa mbali na bendi hizo pia usiku huo burudani itaporomoshwa na mkali wa Mchiriku, Msaga Sumu, Bi Mwanahawa na Wakali Dancers kwa kiingilio cha Sh.7,000 tu.

Leave A Reply