×

Oleksandr Zinchenko kinda aliyemkuna kichwa Pep Guardiola

oleksandr-ukraine-zinchenko_3476405 Na Leonard Msigwa

Oleksandr Zinchenko kinda wa nchini Ukraine anakuwa mchezaji wa mwisho kusajiliwa na kocha wa Manchester City, Pep Guardiola. Manchester City wamekamilisha usajili muhimu kwao wa kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa toka nchini Ukraine. Oleksandr Zinchenko anakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na kocha huyo tangu asaini mkataba wa kufundisha timu hiyo.

Wasifu wake

Umri: 19

Nafasi: kiungo

Klabu : Manchester City

Uraia : Ukraine

Zinchenko akiwa na jezi ya taifa lake kwenye mashindano ya Ulaya 2016

Historia yake

Zinchenko aliichezea timu vijana ya nyumbani kwao ya Shakhtar Donetsk na aliondoka bila kucheza mechi yoyote kwenye timu ya wakubwa. Alienda kufanya majaribio kwenye klabu ya Rubin Kazan, na baadaye alijiunga na klabu ya Ufa.

Hakuwa na msimu mzuri baada ya kupata wakati mgumu kuingia kikosi cha kwanza, alifanikiwa kucheza mechi saba tu kwenye msimu wa kwanza Ufa 2014-2015. Alifanikiwa kucheza mechi 24 msimu wa 2014-2015 na kufanikiwa kufunga magoli mawili na kuisaidia timu yake kushika nafasi ya 12 hadi mwisho  wa msimu.

Zinchenko alichaguliwa kwa mara ya kwanza timu ya taifa Ukraine  mwaka jana na kuweka historia ya kuwa mchezaji wa tatu mdogo kuwahi kuichezea timu hiyo wakati huo akiwa na miaka 18. Alivunja rekodi ya gwiji wa nchi hiyo Adriy Shevchenko kuifungia goli timu ya taifa kwenye ushindi  dhidi ya Romania 4-3 kwenye maandalizi ya kujianda na michuano ya mataifa ya Ulaya. Wakati huo akiwa na umri wa miaka 19 na siku 214.

ukraine-andriy-shevchenko-striker_3416816Zinchenko alivunja rekodi ya gwiji Andriy Shevchenko (pichani).

Kwenye mashindano ya mataifa ya Ulaya aliingizwa akitokea benchi kwenye mechi za makundi ambazo walipoteza dhidi ya Ujerumani na Ireland Kaskazini. Na kwenye mechi ya mwisho ya makundi alianza kikosi cha kwanza ambapo walifungwa goli 1-0 na Poland. Timu ya Ukraine ilihitimisha hatua ya makundi bila kupata pointi wala goli.

Staili yake ya uchezaji.

Ana uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji anayemudu vyema nafasi ya kiungo wa kati au mshambulianji. Staili yake ni kumiliki mpira kwa kutumia mguu wake wa kushoto.

Hajaonesha uwezo wa juu kwenye kufunga magoli, lakini ana uwezo mkubwa sana wa kumiliki mpira na mzuri kwenye kutoa pasi murua na kupiga krosi zenye macho.

Nafasi yake ndani ya Manchester City

Hapewi nafasi kubwa sana kutumika kwenye msimu wa mwaka 2016-2017, amesajiliwa kwaajili ya maendeleo ya baadaye ya klabu. Kocha Pep Gurdiola si muumini mkubwa wa kuwatumia vijana kwenye kikosi cha kwanza. Huenda akatolewa kwa mkopo klabu nyingine kuongeza uzoefu zaidi.

Tujikumbushe

Zinchenko alicheza timu moja na Emmanuel Frimpong kwenye klabu ya Ufa, na kiungo huyo wa zamani wa Arsenal amezungumzia usajili wa Zinchenko kama usajili bora nchini Uingereza na ataisaidia timu yake kutokana na uwezo alionao.

Leave a Comment