SHABIKI namba moja wa FC Kauzu, Ally Omary ‘Chifu wa Masela’ amezidi kuwa kivutio katika mashindano ya Sport Extra Ndondo Cup baada ya juzi kutinga uwanjani akiwa amebebwa ndani ya kibanda chenye muonekano kama wa nyumba kikiwa na vitu kadhaa ndani.
Chifu wa Masela amefanya hivyo katika mchezo wa hatua 16 Bora kwenye Uwanja wa Chuo cha Bandari ‘Wembley’, Dar ambapo timu yake ilishinda bao 1-0 dhidi ya Mlalakuwa Rangers.
Ndani ya nyumba yake hiyo, kulikuwa na simu ya mezani na luninga ya kisasa ‘flat screen’ huku juu ya paa la nyumba hiyo kukiwa na ungo wa King’amuzi cha Azam TV.
Wakati mchezo ukiendelea Chifu huyo aliamua kutoka ndani ya nyumba hiyo na kuzunguka uwanjani peke yeke akiwa anazungumza Kingereza kuhusu timu yake kitendo kilichosababisha shangwe ziongezeke uwanjani hapo.


