×

Kahama: Kibinti miaka 13 chaolewa, chatorokea polisi

pic+majambaziKamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Mika Nyange.

KAHAMA: Kibinti chenye umri wa miaka 13 (jina linahifadhiwa) mkazi wa Kijiji cha Shunu, Kata ya Nyahanga wilayani Kahama, kinadaiwa kuolewa na jamaa aliyefahamika kama baba Saidi (23) lakini baada ya wawili hao kukamatwa, msichana huyo alitoroka akiwa mikononi mwa polisi na hajapatikana hadi sasa.

Baba aliyefahamika kwa jina la Martine, ambaye ndiye mzazi wa binti huyo alitoa malalamiko yake mbele ya shirika la kutetea haki za binadamu lijulikanalo kama Shihabi ambapo alisema mtuhumiwa huyo kazi yake kubwa ni kufyatua matofali na kuwapa ajira watoto wadogo ya kubeba na kuyapanga, kazi ambayo binti yake alikuwa akiifanya baada ya kutoroka shule.

Aliongeza kuwa wakati binti yake akifanya kazi hiyo, kijana huyo alimrubuni akamtorosha na kwenda kuishi naye kama mkewe katika Kijiji cha Kagongwa.

Alidai kuwa, baada ya kumtafuta kwa muda mrefu hatimaye aliweza kumpata mwanaye ambapo aliwakamata wote na kuwafikisha katika kituo cha polisi wilayani hapo, lakini alidai maofisa wa polisi walikuwa hawampi ushirikiano wa kutosha ambapo walimtaka mtoto huyo aende kufuata nguo zake huko kijijini alikokamatiwa na arudi kituoni, lakini baada ya kuondoka hakurejea tena.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Mika Nyange alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema bado halijafika ofisini kwake, lakini akamtaka mlalamikaji huyo kufika kwake ili suala lake liweze kupatiwa ufumbuzi.

Leave a Comment