Waandishi wetu, Risasi Jumamosi
DAR ES SALAAM: Ulinzi na usalama wa maelfu ya wanavyuo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) sambamba na majirani zao, Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) ni kama sifuri tu huku kukiwa na mianya mingi ya watu wanaoweza kuwa na nia mbaya, kupenya bila kugundulika na kutimiza malengo yao, Risasi Jumamosi lina ripoti kamili.
Mapema wiki hii, kikosi maalum cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ cha Giobal kilipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanachuo waliosema kwamba katika siku za karibuni, kumekuwa na wimbi la wizi wa vifaa vyao, zikiwemo laptop na simu, vitendo vinavyofanywa na watu wanaoingia kwenye vyuo hivyo wakitokea mitaani.
UDOKOZI MDOGO
“Kila siku lazima utasikia mtu kaibiwa, muda mwingine wezi wanaingia mpaka hosteli za humu ndani chuoni, wanachukua wanachokitaka na kutokomea, wakati hapa kuna walinzi. Kwa nini eneo lote la chuo lisizungushiwe uzio? Mbona Sua (Chuo Kikuu cha Sokoine- Morogoro) ina eneo kubwa kuliko vyuo vyote Afrika Mashariki lakini eneo lake lote limezungushiwa fensi?
“Tunawaomba mtusaidie kulipigia kelele hili maana usishangae siku yakatukuta makubwa. Ni vyema tukawa watu wa kukinga badala ya kutibu,” alisema mwanachuo mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake huku akiungwa mkono na wenzake.
OFM KAZINI
Baada ya kupata malalamiko hayo, Julai 13, mwaka huu, makamanda wa OFM walijipanga na kufika chuoni hapo kwa lengo la kujiridhisha kama malalamiko ya wanachuo hao yana ukweli wowote!
CHUO KIKUU CHA ARDHI
Awali, Makamanda wa OFM walifika kwenye Chuo Kikuu cha Ardhi ambapo licha ya kuwepo mlinzi mwenye kirungu, aliyekuwa getini, walifanikiwa kuingia kiulaini, wakiwa hawana utambulisho wowote unaowaonesha kama ni wanachuo, wakajichanganya na wanachuo wengine waliokuwa katika pilikapilika za mitihani (huu ni msimu wa kufanya mitihani ya kumaliza mwaka wa masomo).
Kisha OFM walielekea kwenye hosteli za chuoni hapo, wakazurura kwa zaidi ya saa nzima mpaka kwenye vyumba vya ghorofani bila kuulizwa chochote wala kushtukiwa na mtu yeyote.
Baada ya hapo, makamanda walielekea upande wa madarasa (lecture halls) lakini walikumbana na ugumu kidogo kwa sababu yalikuwa yakitumika kwa mitihani, wakaishia kupitapita nje lakini hata hivyo, hakuna aliyeonesha kugundua kwamba, ni OFM na si wanachuo.
OFM KWENYE VIBWETA
Makamanda walielekea kwenye maeneo yenye mabenchi ya zege maarufu kama ‘vimbweta’ yanayotumika kujisomea ambako walikaa kwenye kimbweta kimoja na kuzuga kama wanajisomea huku wanachuo halisi nao wakiwa kwenye vimbweta vingine wakiendelea kujisomea.
Licha ya kukaa kwa zaidi ya saa nzima eneo hilo, hakuna aliyeonesha kuwashtukia. Baada ya hapo, makamanda walihamia kwenye vimbweta vilivyokuwa upande mwingine, ndani ya eneo hilo la chuo ambako nako walijiachia vya kutosha bila kushtukiwa huku askari kadhaa waliokuwepo wakionekana ‘kusinzia’ kiasi cha kushindwa kugundua kwamba makamanda wa OFM walikuwepo eneo hilo.
UBAO WA MATANGAZO
Baada ya hapo, makamanda hao walijichanganya kwenye mbao za matangazo (notice boards) kadhaa ndani ya chuo hicho, nao wakawa wanatazama ratiba za mitihani na matangazo mengine. Walipomaliza walielekea ‘canteen’ ambako nako walikaa kwa dakika kadhaa kabla ya kuamua kuondoka.
Wakati wa kutoka, kama ilivyokuwa wakati wa kuingia, licha ya kuwepo kwa walinzi waliovalia sare, hakuna aliyeonesha kushtukia uwepo wa makamanda hao, vijana wakatoka kiulaini kama walivyoingia.
CHUO KIKUU CHA MLIMANI
Baada ya kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi, makachero wetu walielekea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam almaarufu Mlimani ua UDSM ambapo walipita kwenye geti kubwa la kuingilia bila kuulizwa chochote na askari wawili waliokuwa eneo hilo.
Wakati wa kupita, makamanda wa OFM waligundua kwamba, licha ya askari hao kujitahidi kukagua baadhi ya magari, mengi yalikuwa yakiingia na kutoka bila kukaguliwa jambo linaloweza kuhatarisha usalama.
Hata yale yaliyokuwa yakikaguliwa, askari hao hawakuwa na vifaa maalum vya ukaguzi zaidi ya kuwahoji madereva walichobeba na wanakoelekea, jambo linaloweza kuwafanya watu wenye nia ovu kupitisha silaha kiulaini na kuhatarisha maisha ya maelfu ya wanachuo wa chuo hicho.
VIBWETA TENA
Baada ya kuingia ndani kabisa ya chuo hicho, makamanda wetu walijichanganya na wanachuo wengine wengi kujisomea kwenye ‘vimbweta’ vya maeneo mbalimbali bila kushtukiwa na mtu yeyote, wakijifanya nao ni wanachuo wanaojiandaa na mitihani.
OFM MPAKA MAKTABA
Kama hiyo haitoshi, makamanda wetu waliingia mpaka ndani ya maktaba ya wazi ambako wanachuo wengine walikuwa wakiendelea kuchagua vitabu na wengine wakijisomea, wakazugazuga na baadaye kutoka bila kushtukiwa.
Ziara ya uchunguzi iliendelea ndani na nje ya chuo hicho ambapo mambo mengine matatu hatari kwa usalama wa wanachuo yalibainika:
SAM NUJOMA
OFM ilibaini kwamba, upande ambao chuo kinapakana na Barabara ya Sam Nujoma ya kutoka Mwenge kwenda Ubungo hakuna uzio wala kizuizi chochote jambo ambalo linafanya iwe rahisi kwa yeyote kuingia mpaka ndani ya chuo hicho bila kukaguliwa na mtu yeyote kupitia kwenye njia nyingi za panya.
CHANGANYIKENI
Upande mwingine, chuo hicho kinapakana na makazi ya watu wa eneo la Changanyikeni ambako nako hakuna uzio wala kizuizi chochote jambo linalofanya iwe rahisi kwa watu ambao si wanachuo, kuingia mpaka chuoni bila kipingamizi hata kama mtu huyo ana silaha au kitu chochote cha hatari.
DALADALA NDANI YA CHUO
Zipo pia daladala zinazofanya safari zake kutokea Kimara na Ubungo kuelekea Mwenge na Makumbusho ambazo zinapita ndani ya chuo huku kituo kikubwa kikiwa mita chache kutoka kwenye jengo la utawala!
Abiria wa daladala hizo, ukiachilia mbali wanachuo, ni raia ambao hutokea uraiani na kushuka ndani ya vituo vilivyomo eneo la chuo, wengi wakiwa hawana shughuli za muhimu zaidi ya kwenda kupunga upepo kwenye bustani za chuo.
Baada ya ziara hiyo iliyochukua zaidi ya saa 24 kwani makamanda hao walilazimika kuondoka siku ya kwanza baada ya giza kuingia na kurejea siku iliyofuata, waliwasilisha ripoti ya walichokibaini kwa kamanda wao mkuu.
MAMLAKA HUSIKA
Baada ya ripoti hiyo kutua kwenye dawati la Risasi Jumamosi, waandishi wetu walifanya jitihada za kuzungumza na mamlaka zinazohusika kusimamia ulinzi ndani ya chuo hicho. Mmoja wa walinzi wa chuo hicho, aliyekataa kutaja jina lake, alisema mwenye mamlaka ya ulinzi ni uongozi wa Chuo Kikuu, hivyo ni bora kumtafuta Ofisa Habari wake.
Gazeti hilo lilifika ofisini kwa Ofisa Habari wa Chuo, Isidori Shirima ambaye hata hivyo hakuwepo ofisini na habari zilizopatikana baadaye, zinasema mkuu huyo wa kitengo cha habari yupo nje ya nchi kimasomo. Maofisa wengine wote walioombwa kutoa maoni yao juu ya jambo hilo walikataa kwa maelezo kuwa suala hilo linapaswa kuzungumzwa na mamlaka zinazohusika.
NENO LA MHARIRI
Lengo la habari hii si kukosoa, bali ni kushauri. Kinga ni bora kuliko tiba! Ni muhimu mamlaka husika zikachukua hatua za haraka kuhakikisha ulinzi unaboreshwa kwenye maeneo hayo. Inawezekana kabisa eneo lote la vyuo hivyo likawekewa uzio, wanachuo wakawa na vitambulisho shingoni huku askari wakiongeza umakini kuhakikisha kila anayeingia au kutoka ndani ya maeneo ya vyuo anajulikana nia yake.


