JE, una umri usiozidi miaka 36 tangu uzaliwe? Kama jibu ni “ndiyo’ basi ujue ulizaliwa baada ya Rais Jose dos Santos wa Angola kuingia ikulu ya nchi hiyo Septemba 10, 1979! Rais huyo bado yuko madarakani hadi leo na ni mmoja wa viongozi matajiri zaidi Afrika na duniani.
Rais Santos alikuwa ni miongoni mwa marais wa kusini mwa Afrika waliopitia mikononi mwa utawala wa Julius Nyerere ambaye alikuwa akiwaunga mkono katika vita vyao vya kujikomboa na alikuwa amewapa hata makazi hapa nchini wakati wakipigania uhuru wa nchi zao. Ni miongoni mwa “wapiganaji” wa Afrika waliobadilika baada ya kuingia ikulu ya nchi zao.
Kuna baadhi ya viongozi waliopitia Tanzania wakati wa Mwalimu Nyerere, wakaenda katika nchi zao, wakatawala kwa uadilifu huku wakikwepa kupora mali za wananchi wenzao kwa kujilimbikizia mali.
Hivi sasa, Rais Dos Santos ni kiongozi wa pili katika Afrika kwa kukaa katika ikulu ya nchi yake kwa miaka mingi zaidi. Amekaa madarakani kwa muda wa miaka 36, akiwa ametanguliwa na Rais Teodor Obian Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea ambaye aliingia ikulu ya nchi yake miezi miwili kabla, naye akingali madarakani hadi leo!
Dos Santos aliingia madarakani baada ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wa harakati za kupigania uhuru wa Angola, Agostinho Neto, ambaye aliwahi kuishi jijini Dar es Salaam, huko Kurasini, wakati akiwaongoza wenzake kuung’oa utawala wa Wareno nchini mwao chini ya chama ambacho kwa Kireno kilijulikana kama Movimento Popular de Libertação de Angola (MPLA).
Wakati huo, Dos Santos alikuwa ni kijana wa miaka 37 aliposhika madaraka ya urais na kuwa kiongozi wa MPLA, chama ambacho kimeitawala nchi hiyo peke yake tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Wareno mwaka 1975. Ni mmoja wa vijana wa Angola waliosomea Urusi ya Kisoviet.
Kukaa madarakani miaka mingi huathiri akili hata za malaika. Kwa mujibu wa Jarida la Forbes, binti wa rais huyo aitwaye Isabela dos Santos ndiye mwanamke tajiri zaidi barani Afrika na ni mmoja wa wanawake matajiri zaidi duniani. Ikumbukwe kwamba Angola ni moja ya nchi zinazozalisha petroli duniani ambayo inachimbwa kwa wingi eneo la Cabinda na ina utajiri wa madini kibao yakiwemo almasi!
Wachunguzi wasiopenda kudanganywa wanauhusisha utajiri huo wa Isabela na baba yake – Rais Santos.
Hayo yametokea katika utawala wake ambao unasemekana ni moja ya tawala zinazoongoza kwa rushwa barani Afrika ambapo asilimia 70 ya watu wake wanaishi maisha ya kimaskini licha ya kuwa na petroli ya kumwaga.
Dos Santos aliyesomea uhandisi wa petroli na mawasiliano ya radar, ameoa mara tatu na ana watoto sita. Mmoja wa wake zake akiwa mama wa Isabela ambaye ni Mrusi.