×

Zijue sababu za watoto kuharisha -2

Little boy with stomach pain
Little boy with stomach pain

Inaendelea toka wiki iliyopita

Watoto wachanga chini ya miezi 3 wanapata sehemu ya kinga (Antibodies) kutoka kwa mama anayenyonyesha na vilevile kinga mtoto aipatayo kupitia kondo la nyuma (Placenta) kabla ya kuzaliwa. Kwa maana hiyo basi shambulizi la awali baada ya miezi 3 lina uwezekano wa kusababisha ugonjwa mkali zaidi.

MUONEKANO WA MGONJWA

Watoto wanaohara kwa sababu ya Rotavirusi huwa na dalili kuu tatu ambazo ni homa, kutapika na kuharisha. Kawaida choo kinakuwa cha majimaji.

Wakati mwingine kuharisha kunaweza kujitokeza baadaye baada ya kutapika au homa. Joto la mtoto huwa si kali sana ingawa baadhi ya watoto wanaweza kuwa na joto kali linalozidi nyuzi joto 39 za sentigredi. Kutapika kunaweza kusiwe zaidi ya saa 24.

Inashauriwa kuchunguza kiasi cha maji kilichopotea. Iwapo uzito wa mtoto utakuwa umepungua kwa zaidi ya asilimia 10, mtoto anaweza kuwa na dalili kama kupoteza fahamu, kuwa na mapigo ya moyo ya kasi, kushindwa kula na kunywa, kuwa na macho yaliyolegea na kuingia ndani sana (Severe Sunken Eyes), kushindwa kutoa mkojo kabisa, kutotoa machozi na mdomo kuwa mkavu.

Upungufu wa kati ya asilimia 5-10 ya maji mwilini, husababisha macho ya mtoto kuingia ndani (Sunken Eyes), ngozi kurudi taratibu pindi inapovutwa (Loss of Skin Turgor), mapigo ya moyo kuwa kasi, kuwa na ubonyeo katika sehemu ya mbele ya kichwa (Depressed Anterior Frontanele).

Unapoona dalili hizo wakati mtoto wako anaharisha unapaswa kumpeleka haraka kituo cha afya ili kupata ushauri wa wataalam wa afya.

MATIBABU

Ingawa yawezekana mtoto kupona bila hata matibabu lakini ni jambo muhimu kuchunguza madhara yanayoweza kusababishwa na upungufu wa maji mwilini.

Ieleweke kuwa watoto wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupungukiwa na maji mwilini kutokana na kuharisha, hivyo basi msingi wa matibabu ni kurudisha kiasi cha maji kilichopotea.

Hali kadhalika, matumizi ya madini ya zinc yamehusishwa na kupungua kwa makali ya ugonjwa na kupunguza muda wa kuharisha.

ORS ambayo ni mchanganyiko wenye uwiano mzuri wa chumvi na sukari ni aina ya tiba inayopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya matibabu.

Uwiano uliopo katika ORS huwezesha utumbo wa mtoto kufyonza vizuri maji na madini mengine.

Leave a Comment