KWAKO Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule ‘Prof Jay’ habari yako. Pole na majukumu ya kila siku, vipi familia yako haijambo?
Binafsi namshukuru Mungu, naendelea kupambana na maisha yangu niliyochagua ya uandishi wa habari. Kila siku hapa ni kusaka habari mpya na kuwajuza mashabiki wetu wa burudani, kila kinachoendelea.
Nimekukumbuka kwa barua leo mheshimiwa usiyependa kuitwa mheshimiwa. Labda nikuite mtumishi kama unavyofurahia zaidi mwenyewe. Mtumishi nafahamu jinsi gani mlivyopambana kuhakikisha Muziki wa Bongo Fleva unasonga mbele.
Nafahamu jinsi ulivyopambana kwa namna moja au nyingine kuwafanya wazazi wawaruhusu vijana wao waingie kwenye muziki huo. Mlithubutu na mkafanikiwa. Awali, mlionekana wahuni lakini baadaye mlieleweka na sasa muziki huo ni biashara.
Mtumishi, ninapozungumzia biashara ya muziki kama zilivyo biashara nyingine, una changamoto zake. Ukiwa kama mkongwe, najua unafahamu kinagaubaga changamoto zake. Wewe umepitia milima na mabonde yake.
Mtumishi, suala la wizi wa kazi za wasanii unajua ni tatizo. Wasanii kuwa na haki miliki, malipo ya kazi zao kwenye redio na matamasha mbalimbali bado ni changamoto. Wiki iliyopita ulinukuliwa katika Global TV ukizungumzia baadhi ya changamoto hizo.
Ukasema kwamba tatizo wasanii wamekuwa wakishindwa kupata haki yao kwa sababu hawana umoja. Kwamba kila mmoja anapigana kivyake katika kutetea masilahi yake. Ukasema kwamba kila linapokuja suala la pamoja, kunakuwa na mpasuko miongoni mwao.
Mtumishi, nataka nikuambie kwamba, unapaswa kuamua sasa kushughulikia suala hilo. Kujenga umoja ni jambo ambalo haliwezi kukushinda. Wewe sasa una kofia mbili, mbunge lakini pia ni msanii. Una fursa kubwa ya kushawishi mamlaka mbalimbali zinazohusika.
Una nguvu ya kuwaambia wasanii wawe kitu kimoja. Watengeneze umoja utakaokuwa na nguvu na kuweza kutambulika na serikali. Utakaosikilizwa kwa hoja. Serikali iweze kushughulikia matatizo yenu kwa umoja.
Mtumishi, wewe mwenyewe ulisema kwa sasa vijana mpo wengi bungeni, kuna mheshimiwa Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ wa Mbeya Mjini ambaye alikutangulia. Ndiye aliyekupa nguvu wewe kuingia kwenye siasa, tengenezeni umoja wa kweli ambao mtauasisi nyinyi ili iwe rahisi wasanii kuwasikiliza.
Nyinyi mnajua matatizo yaliyopo kwenye gemu, pambaneni ili Bongo Fleva iwe na nguvu. Masilahi ya wasanii yawe yanajadiliwa kama kazi nyingine yoyote ile. Haki miliki iwe kweli inakwenda kwa msanii husika. Ilindwe.
Mtumishi, mapambano yako ya awaili yalikuwa yanakosa meno kwa kuwa tulikuwa tunaongelea huku mtaani. Sasa hivi upo mjengoni katika chombo cha kutunga sheria. Upo jirani na mawaziri husika. Mnakutana muda wowote, piganieni miswada mtakayoamini inawatetea wasanii.
Nyinyi muwe mfano wa kweli kwa kuunganisha nguvu ya pamoja kwa wasanii, baadaye muwe na sauti moja ambayo itasikika kwa serikali na kupata matokeo chanya.
Ni matumaini yangu utaifanyia kazi barua hii na mambo yatabadilika, nikutakie mafanikio mema katika utendaji wa kazi zako za kila siku.
Mimi ni ndugu yako;