Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers Ltd, Eric Shigongo, akihutubia katika ukumbi wa Victory Christian Centre ulioko Mbezi Beach jijini Dar es Salaam katika semina ya ujasiriamali kuhusu ‘Mbinu za Kufanikiwa Kwenye Kipindi Kigumu cha Uchumi’.
Mmoja wa wanasemina akinyoosha mkono kuuliza swali.
Semina ikiendelea.
Wanasemina wakisikiliza kwa makini kilichokuwa kikiendelea ukumbini.
Shigongo akibadilishana mawazo na baadhi ya washiriki wa semina.
MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers Ltd, Eric Shigongo, jana alitoa somo kuhusu mbinu 10 za kufanikiwa wakati wa kipindi kigumu cha uchumi.
Shigongo aliyasema hayo jana kwenye semina maalum iliyofanyika katika Ukumbi wa Victory Christian Center uliopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa katika kipindi kigumu cha uchumi, kuna watu wanatengeneza utajiri huku wengine wakifilisika, wengine wakifukuzwa kazi na wengine wakipandishwa vyeo.
Mambo aliyoyataja kuwa yanafaa kuzingatiwa katika kipindi kigumu ni kutoingiwa na hofu, kulichambua tatizo, kubadilika kuendana na wakati na kuwa na msimamo na lengo lako.
Mbinu zingine alizosema ni kuongeza ubunifu zaidi wa biashara, kujiwekea tabia njema na kuwa na vyanzo vingi vya mapato vinavyoendana na wakati huo.
Pia alisema mbinu nyingine ni kuhifadhi na kununua bidhaa nyingi zinazokuwa zikiuzwa na watu, kuhakikisha unaongeza matangazo ya shughuli unazozifanya ili watu watazame bidhaa zako, kuweka mahusiano yako karibu na Mungu ili akusaidie kwa uyatakayo.
Vilevile aliyatolea ufafanuzi yote aliyowafundisha jinsi yanavyoweza kumsaidia mtu katika kipindi kigumu cha uchumi na kukabiliana na hali hiyo ya maisha.
Aidha kipengele cha kuhifadhi na kununua bidhaa nyingi, alisema mtu anachotakiwa kufanya ili biashara yake iimarike ni kununua bidhaa zinazouzwa kwa kipindi hicho na watu wengine mfano nyumba ambazo zinakuwa zinauzwa kwa bei ya chini ambapo baadaye wakati uchumi ukiimarika, mtu anaweza kuziuza na kapata faida zaidi.
Mkurugenzi huyo alihitimisha kwa kuwashukuru watu wote waliohudhuria semina hiyo huku akiamini kuwa watakuwa wamepata somo jema na kuweza kukabiliana na nyakati.
Semina hiyo ilikuwa ikitolewa bure na kwa kujua hotuba yote aliyoitoa, tembelea Youtube na Subcribe Channel ya Global TV Online.
Stori: Denis Mtima / GPL





