×

Waziri Ngonyani ataka fidia ya bilioni moja

NGONYANI (1)Naibu Waziri  wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mhandisi Edwin  Ngonyani.

Dar es Salaam

NAIBU Waziri  wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, ambaye ni mbunge wa jimbo la Namtumbo Mhandisi Edwin  Ngonyani, anataka kulipwa fidia ya shilingi bilioni moja kutoka kwa gazeti moja linalotoka kila wiki, kwa madai ya kuchapisha habari ambazo zimemchafua.

NGONYANI (2)Akizungumza na wanahabari ofisini kwake leo jijini Dar, Naibu Waziri Ngonyani amesema gazeti hilo, Agosti 4, mwaka huu, liliandika habari iliyosomeka “Waziri amchafua JPM” ikimhusisha na upokeaji wa fedha kutoka kampuni moja ya madini wakati akiwa Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico).

Alisema amewaandikia notisi ya siku saba kuwataka waombe radhi na kumlipa fidia, vinginevyo atawapeleka mahakamani mwandishi wa habari hiyo, wamiliki wa gazeti hilo pamoja na mchapaji wake.

NGONYANI (3)Waandishi wa habari wakifuatilia mkutano huo.

Mhandisi huyo alisema habari hiyo haikuwa ya kweli, kwani mwandishi wake alitumia nyaraka za kugushi, ikiwemo barua iliyoandikwa na kutiwa saini ikimuonyesha yeye kama Kaimu Mkurugenzi wa Stamico, wakati tarehe iliyoonyeshwa kwenye barua hiyo, yeye alikuwa ni Mkurugenzi kamili.

Alidai habari hiyo imewachafua watu wengi ikiwemo familia yake, wapiga kura wake ambao walijitoa kumsaidia wakati wa kampeni na hali kadhalika zimemchafua Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumhusisha na fedha kutoka kwa wawekezaji wa nje kwa kuwaahidi kuwa mitaji yao nchini itakuwa salama.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alishasema kama kuna mfanyabiashara yeyote aliyechangia kuingia kwake ikulu, ajitokeze na hakuna aliyefanya hivyo, Iweje leo mtu anaibuka na kuandika habari za kugushi?” alisema.

PICHA NA DENIS MTIMA/GPL

Leave a Comment