×

Tanzania, Kongo kufanya kongamano la pamoja

TANZANIA kwa kushirikiana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinatarajiwa kufanya kongamano la pamoja  la kibiashara kujadili ongezeko la biashara na fursa za uwekezaji na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika kuchunguza fursa mbalimbali za kiuchumi.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo, mratibu wa kongamano hilo, Anna Msonsa alisema kuwa kongamano hilo linatarajiwa kufanyika Septemba 22 mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa FEC jijini Lubumbashi, Kongo huku likiwa na lengo la kuwaweka pamoja waendeshaji wakubwa wa sekta binafsi kutoka hapa nchini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pia litajadili kuhusu kuwekeza katika kilimo cha biashara.

Alisema nchi hiyo imekuwa ikionyesha nia kubwa kwenye utafutaji wa nishati na madini katika sekta ya mafuta na gesi nchini hasa kwa kuzingatia mkutano uliofanyika Agosti mwaka huu uliokuwa na mapendekezo ya kuwezesha Jiji la Kinshasa kuuza mafuta kupitia mfumo wa bomba linalotoka bandari ya Tanga hadi Hoima nchini Uganda.

Alifafanua kuwa kongamano hilo litakuwa likifanyika kila mwaka na limekuja baada ya ukuaji wa uchumi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufikia asilimia 7.7 kipindi cha mwaka 2015 na yote hayo ni kutokana na nguvu ya viwanda vya madini na uhusiano wa uwekezaji.

Kauli mbiu ya kongamano hilo mwaka huu inasema,: “Kuimarisha mahusiano ya kibiashara na fursa za uwekezaji baina ya nchi hizi mbili,” na linatarajia kukusanya wafanyabiashara wakubwa zaidi ya 100 kutoka sekta binafsi za Tanzania na Kongo.

 1Mratibu wa kongamano hilo kutoka Chama Cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo  Tanzania (TCCIA), Anna Msonsa (kulia) akizungumza na wanahabari.

2-001Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania, (TPSF), Lous Accaro ambaye pia ni mmoja wa waandaji wa kongamano, akifafanua jambo.

3-001Meneja Masoko wa Kampuni ya GSM, Farida Lubanza (kushoto) ambaye ni miongoni mwa wadhamini wa tamasha hilo akielezea jambo. 

4Wanahabari wakichukua tukio hilo.

Na Denis Mtima/Gpl