
Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, ameamua kujibu kile kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii katika siku za karibuni.
Nasikitishwa sana na matumizi mabaya ya picha zangu mtandaoni hususan watu kunilisha maneno kwa kutaka kutimiza malengo yao ya kisiasa.
— Jakaya Kikwete (@jmkikwete) October 27, 2016
Usiku wa kuamkia leo, kupitia akaunti yake ya Twitter, Kikwete aliandika masikitiko yake juu ya namna watu wanavyotumia picha zake na kupotosha yale aliyoyasema juzi akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kufanikisha matwaka yao ya kisiasa.
Nimestaafu naomba niachwe nipumzike. Nisingependwa kuhusishwa na siasa za mtandaoni dhidi ya Serikali. Namuunga mkono Rais na Serikali yake.
— Jakaya Kikwete (@jmkikwete) October 27, 2016
Aidha, Kikwete aliwataka watu hao kumuacha kwani ameshamaliza muda wake wa uongozi hivyo ni wakati wake sasa kupumzika.
Kikwete pia alikanusha tuhuma za kuwa ana tofauti na Rais wa sasa Dkt John Pombe Magufuli na kusema kuwa anamuunga mkono na serikali yake.
Kauli ya Kikwete ambayo imekuwa ikipotoshwa mtandaoni ni ile aliyoitoa kwenye maadhimisho ya miaka 55 ya chuo kikuu hicho ambapo aliwataka viongozi wapya kuenzi mazuri ya nyuma akimaanisha kwamba hivi sasa yeye ndiye Mkuu wa Chuo hicho (Chancellor), hivyo akaahidi kuyaenzi mazuri aliyoyakuta kutoka kwa watangulizi wake.
“Ukiwa mpya lazima watu waone una mambo mapya, lakini mapya ya maendeleo,” alisema Kikwete na kuongeza: “Siyo mapya ya kubomoa ya kule tulikotoka,”