×

Lwandamina Aachia Zesco, Aanika Anakoelekea Baada ya Hapo

lwandamina-2Lusaka, Zambia: KOCHA Mkuu wa Klabu ya Zesco United ya Zambia, George Lwandamina amejiuzulu nafasi yake hiyo jana baada ya kuandika barua kwa uongozi wa klabu hiyo akiomba kuachia ngazi nafasi yake hiyo.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu, Justin Mumba na Ofisa Habari wa klabu hiyo wamethibitisha kupokea barua ya Lwandamina ya kuomba ajiuzulu kazi yake hiyo klabuni hapo huku akieleza kuwa sababu ya kuchukua uamuzi huo ni kuwa anataka awe free kwa ajili ya kufanya mambo yake.

“Ni kweli Lwandamina amejiuzulu. Tumepokea email yake leo asubuhi lakini hajataja sababu yeyote ya msingi ya kufikia uamuzi huo,” amesema Banda ambaye ni manager wa Zesco United.

Klabu ya Zesco imetoa taarifa rasmi kupitia ukurasa wao wa facebook wakithibitisha kuachana na kocha huyo ambaye wiki chache zilizopita alikuwa Dar es Salaam na kuhusishwa kutaka kujiunga na klabu ya Yanga hadi kupelekea kocha mkuu wa Yanga kutangaza kujiuzulu.

“Kocha mkuu wa Zesco United George Lwandamina amejiuzulu nafasi yake asubuhi ya leo, klabu imepokea na kuikubali barua yake ya kujiuzulu na kumshukuru kwa mchango wake pamoja na kazi yake aliyoifanya akiwa kocha wa Zesco United,” inasomeka taarifa ya Zesco United iliyotolewa kupitia ukurasa wao wa facebook.

Lwandamina alijiunga na Zesco mwaka 2004 na kufanikiwa kushinda mataji mawili ya ligi, kombe moja la Barclays, Ngao ya Jamii na kuiongoza timu hadi hatua ya nusu fainali ya CAF Champions League mwaka 2016.

Klabu imemteua aliyekuwa  kocha msaidizi Tenant Chembo kuchukua nafasi ya Lwandamina hadi mwisho wa msimu huu.

Kocha George Lwandamina amesema baada ya kuachia ngazi kuinoa Zesco ya Zambia sasa yuko tayari kwa kazi mpya.

Lwandamina amezungumza moja kwa moja na tovuti hii kutoka Lusaka, Zambia na kusema: “Niko tayari kwa kazi mpya”.
“Kweli niko tayari kwa kazi mpya, lakini siwezi kusema ni wapi,” alisema.
Alipoulizwa tayari kuna taarifa za uhakika anakuja nchini kwa ajili ya kuinoa Yanga, alisema:
“Kweli? Kama itakuwa hivyo si kitu kibaya. Lakini naweza kukuhakikishia niko tayari kwa kazi mpya.”
Kocha huyo ameondoka Zesco kwa kuachia ngazi na ndiyo anatua nchini kesho alfajiri kwa ajili ya kuinoa Yanga na kuchukua nafasi ya Hans van der Pluijm.