Aliyewahi kuwa Waziri wa Elimu na Mbunge wa Mufindi Kaskazini (CCM), Joseph james Mungai amefariki dunia jioni hii katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtoto wa marehemu aitwaye, Geofrey Mungai imeeleza kuwa marehemu alikimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya hali yake kubadilika ghafla na kuanza kutapika mfululizo na kudhaniwa kwamba alikuwa amekula kitu kisichokuwa kizuri.

Ukithibitisha kifo cha Mungai, uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili umeueleza mtandao huu kwamba marehemu Mungai alifariki saa 11:20 jioni na mwili wake kwa sasa umehifadhiwa katika mochwari ya hospitali hiyo.
Wakati wa harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka jana 2015, mwanasiasa huyo aliyezaliwa Oktoba 24, 1943 alikihama chama chake cha CCM na kujiunga na CHADEMA.

Miongoni mwa mambo ya kukumbukwa kwa marehemu Mungai ni pamoja na maamuzi yake wakati akiwa waziri wa elimu ambapo aliamua kuunganisha masomo ya Fizikia na Kemia na kuyafanya kuwa somo moja liitwalo “Physics with Chemistry” huku akiyafutilia mbali masomo ya biashara mashuleni pamoja na kufuta kabisa mashindano ya michezo mashuleni yaani Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari (UMISSETA) na Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA)
Mwenyezi Mungu Ailaze Roho Yake Mahala Pema Peponi. AMEN
