The House of Favourite Newspapers

AFYA YA LISSU GUMZO 2020!

MIONGONI mwa matukio yaliyozungumzwa sana tangu mwishoni mwa mwaka 2017 mpaka sasa ni kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na masikio ya wengi yamekuwa yakitamani kujua anaendeleaje.

Picha, video, sauti na habari zinazomhusu mwanasiasa huyo aliyeshambuliwa kwa risasi zaidi ya 28, Septemba 7, mwaka jana, mara nyingi zimekuwa gumzo lakini kubwa zaidi ni kusambaa mitandaoni kwa picha na video za hivi karibuni zinazomuonesha Lissu akifanya mazoezi ya kutembea ambazo zimekoleza mijadala juu yake.

Ufuatiliaji wa Risasi Tangu Lissu ashambuliwe kwa risasi na wasiojulikana, nyumbani kwake Area D, jijini Dodoma, Risasi limekuwa likifuatilia siyo tu hali ya afya yake lakini pia na namna watu wanavyomuongelea ambapo muonekano wake mpya wa afya umeibua mengi likiwemo suala la uchaguzi wa mwaka 2020.

Pengine kwa fikra za wengi hawakutarajia kumuona mwanasiasa huyo akiimarika kwa kiwango alichonacho kutokana na mfululizo wa oparesheni zilizotokana na majeraha ya risasi na hivyo kumkatia tamaa za kumudu mambo ya siasa, lakini sasa upepo unaonekana kugeuka kwa kasi.

“Kama yuko hivi inatia moyo sana, habari njema kwa sisi wafuasi wake, viva Lissu viva kamanda tukutane 2020,” ilisema moja kati ya posti iliyowekwa kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram iliyoambatana na picha za Lissu akiwa amesimama akifanya mazoezi.

KWA NINI AFYA YA LISSU NA 2020?

Uchunguzi unaonesha kuwa Lissu ni mwanachama mwenye nguvu ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na amekuwa akisemwa kumudu kushika hata wadhifa wa uenyekiti ambao kwa sasa unashikiliwa na Freeman Mbowe.

Awali hata kabla ya kushambuliwa, vyanzo vya habari kutoka ndani ya Chadema vilisema kuwa kuna baadhi ya wanachama na hasa vijana walikuwa na mkakati wa chinichini kuhakikisha kuwa Lissu anagombea urais wa 2020 au anakuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Kuaminiwa kwake kulitokana na kile kinachoelezwa na wafuasi wake kuwa anaweza kukifanya chama kuwa imara na hata kushika dola kwenye uchaguzi ujao endapo mgombea urais aliyepita Edward Lowassa atawekwa kando kwa kile kinachotazamwa kuwa ni kuchoka kimwili.

Waliokuwa wamemkatia tamaa Lissu kwamba hangeweza kuimarika wamerudisha mioyo nyuma na kwamba sasa moto wake uliokuwa umefifia ndani ya chama chake umewaka upya na kufufua matumaini mapya kwa wananchi wa jimboni kwake na wale wanaompigia chepuo la uongozi mkubwa ndani ya chama.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema, ndani ya Chadema ya leo anakosekana mtu mwingine mwenye ushawishi na kwamba Lissu angalau anaweza kufananishwa na nguvu walizokuwa nazo Dk Wilbroad Slaa, Zitto Kabwe ambao kwa sasa wamehama chama hicho.

WATAALAMU WANASEMAJE?

Hata hivyo, watalaamu wa mifupa wameeleza kuwa kutokana na oparesheni alizofanyiwa na kuvunjika kwa baadhi ya mifupa ya viongo vyake mbunge huyo wa Singida anaweza kuwa fiti kwa uchaguzi ifikapo 2020.

“Wanachofanya madaktari ni kuurudisha mfupa mahala pake kama haujaharibika,” alisema Dk Lukas Thomas wa jijini Dar.

Alipoulizwa kwa uzoefu wake, waliofanikiwa kuungwa mifupa imekuwa ikichukua muda gani alijibu: “Kuanzia miezi sita hadi mwaka inategemea na hali ya mgonjwa mwenyewe.”

Daktari mwingine ambaye hakutaka kutajwa gazetini alieleza kuwa kuunga kwa mifupa iliyovunjika huchukua muda mrefu na hivyo kuwafanya watu waugue kwa kipindi kirefu na kushindwa kuendelea na kazi zao.

“Lakini kuna mbinu za kusaidia kuharakisha kuunga kwa mifupa iliyovunjika ambazo zikifuatwa zitasaidia watu kupona haraka, ulaji wa vyakula vyenye vitamini D ,C na K unahitajika kwa wingi kuharakisha kuunga kwa mifupa iliyovunjika.”

STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.