The House of Favourite Newspapers

Ajibu Aipa Mchongo Yanga

Ibrahim Ajibu.

UONGOZI mpya wa Yanga upo kwenye mchakato wa kuboresha mikataba ya wachezaji wao kwa kuhakikisha wanakuwa na muda mrefu kwa hofu ya kujitokeza kama ya kiungo wao mshambuliaji, Ibrahim Ajibu.

 

Ajibu ni kati ya wachezaji 14 wanaotarajiwa kumaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu (Mei 28), na kiungo huyu fundi anatarajiwa kwenda TP Mazembe ya DR Congo ambayo imeshamtangazia ofa nono.

 

Lakini kiungo huyo atajiunga na Mazembe kama mchezaji huru, baada ya Yanga kujisahau hadi kushtukia anamaliza mkataba wake, kwa hiyo haitaambulia hata shilingi kutoka kwa nyota huyo kama akimalizana na Wacongo hao. Suala hilo limeishtua Yanga na kuamua kuboresha mikataba ya wachezaji wao muhimu akiwemo kiungo mkabaji tegemeo, Feisal Salum ‘Fei Toto’.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema kuwa wamepanga kuipitia mikataba ya wachezaji hivi karibuni kwa ajili ya kuiboresha ili kuepuka kilichotokea kwa
Ajibu ambaye anakwenda Mazembe bure kama mchezaji huru.

 

Mwakalebela alisema, Yanga imepanga kufanya uamuzi huo wa haraka kwa baadhi ya wachezaji ambao mikataba yao inamalizika kwa hofu ya kuwapoteza kama ilivyojitokeza kwa Ajibu. “Ajibu ametupa changamoto viongozi wapya tulioingia madarakani baada ya kuondoka kwake Yanga kama mchezaji huru bila ya klabu kunufaika katika mauzo yake.

 

“Kiungo wetu huyo hivi sasa yupo kwenye mazungumzo na klabu kubwa ya Mazembe iliyoonyesha nia ya kumhitaji kwa ajili ya kumsajili kama mchezaji huru.

 

“Ajibu anaondoka bure klabu ikiwa haijanufaika na mauzo yake, hivyo basi hatutaki hilo lijitokeze tena kwenye klabu yetu ya Yanga, tumepata funzo na viongozi tumepanga kukutana kwa ajili ya kulifanyia kazi hilo kwa kuanza kupitia mikataba ya wachezaji wetu wote,” alisema Mwakalebela.

 

Wachezaji wa Yanga ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu ni Ramadhani Kabwili, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Pato Ngonyani, Gadiel Michael, Abdallah Shaibu, Said Juma na Matheo Anthony. Wengine ni Mrisho Ngasa, Thabani Kamusoko, Papy Tshishimbi, Raphael Daudi, Pius Buswita, Juma Mahadhi, Baruani Akilimali, Amissi Tambwe, Haruna Moshi na Ajibu mwenyewe..

Comments are closed.