The House of Favourite Newspapers

ALICHOFANYIWA MASELE WAFANYIWE MDEE NA LEMA

MIGOGORO ambayo imekuwa ikiibuka bungeni, baina ya baadhi ya wabunge hasa vijana na kiti cha spika na kamati yake ya maadili, inaweza kupatia ufumbuzi kwa njia moja tu ya maridhiano na msamaha.

Nasema hivyo kwa sababu jambo hili limedhihirika katika mgogoro wa hivi karibuni kati ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP).

 

Spika alitangaza kumrejesha nchini Masele ambaye alikuwa anaongoza vikao vya PAP nchini Afrika Kusini, vilivyokuwa vinashughulikia kashfa ya unyanyasaji watumishi kijinsia ya Rais wa Bunge la PAP, Roger Dang.

Mgogoro huu wa Rais wa PAP, Dang unamng’arisha Masele na Tanzania kwa jumla kutokana na msimamo wake katika kupinga matendo ya unyanyasaji wa kijinsia katika chombo hicho, lakini huku kwetu ulimtia matatani.

 

Masele ambaye ni mbunge kijana, alirudi nyumbani kwa wito wa spika na kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoshughulika na maadili kwa tuhuma za kugombanisha mihimili ya nchi wakati akijaribu kujitetea kuhusu wito wa kurudi nyumbani.

Mbunge Masele baadaye alirudi nchini na hatimaye alihojiwa na akatiwa hatiani kwa makosa manne kwanza kudharau mamlaka ya Bunge, kudhalilisha Bunge, kuchonganisha viongozi na kusafiri bila kibali cha spika wa Bunge.

Kamati hiyo pia ikapendekeza Masele asimamishwe kuhudhuria mikutano mitatu baada ya kumtia hatiani.

 

Hata hivyo, baada ya kupewa fursa ya kujitetea, Masele alieleza kilichotokea katika Bunge la PAP na jinsi alivyoamini kuwa alikuwa sahihi na aliomba radhi Bunge na kiti cha spika kwa kilichotokea.

Hata hivyo, licha ya Masele kuibua malumbano mapya na spika, Spika Ndugai kwa busara aliomba Bunge kupuuza hoja za Masele akimweleza kama amekuwa na tabia za ajabu za ‘fitina, uchonganishi, ujanjaunja’ jambo ambalo si zuri na akaamua asamehewe.

 

Watanzania walio wengi wameridhishwa na maamuzi ya Ndugai kumsamehe Masele ingawa bado suala hili lina wingu zito machoni mwa wengi.

Licha ya msamaha huo, hadi sasa haijulikani dhahiri ni nini chanzo cha mgongano huu baina ya Ndugai na Masele.

Itoshe kuheshimu busara za wabunge wetu na kiti cha spika kuamua kulimaliza jambo hili kwa maridhiano ili mambo mengine ya msingi yaendelee. Nawapongeza kwa hili.

 

Tofauti na matukio ya wabunge wengine waliowahi kutiwa hatiani na kamati hiyohiyo, Masele aliomba radhi mapema kabisa, ingawa aliamua pia kuweka mambo mezani akitaka kumbukumbu za kikao cha kamati ziwekwe wazi.

Naamini katika kurejesha maridhiano, upendo na mshikamano katika Bunge ni vyema pia wabunge wengine waliotiwa hatiani kwa makosa mbalimbali wapatiwe msamaha kama wa Masele.

 

Najua hili ni jambo ambalo linapaswa kufuata taratibu kadhaa za kibunge, lakini kwa busara ambazo zilioneshwa na wawakilishi wetu bungeni bila kujali itikadi zao, ni vizuri msamaha ukawagusa na wengine ili warejee kufanya kazi walizopewa na waliowachagua.

 

Nimalizie kwa kulishauri Bunge letu, zile huruma na busara ambazo zimefikia kumsamehe Masele pia zitumike kuwasamehe Profesa Mussa Asaad, Godbless Lema (Arusha-Mjini) na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Nakumbuka hata Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda aliwahi kusamehewa baada ya kuitwa kwenye kamati hiyo ya Bunge.

 

Nimuombe Spika Ndugai, afanye kama alivyofanya kwa Masele na Makonda, naamini ataungwa mkono na wananchi wengi wakiwemo wapiga kura wa wabunge waliosimamishwa na wafanyakazi wa CAG ambao bosi wao amefungiwa milango na Bunge.

Kwa kufuata ushauri huu naamini spika atakuwa juu zaidi.

Na Elvan Stambuli | SIASA ZA SIASA | Simu: 0655-339616

 

Comments are closed.