Angalia Ubunifu Wa UDSM Kutengeneza Nguo Na Nishati Ya Kupikia Kwa Kutumia Mabaki Ya Plastiki
Dar es Salaam 5 Julai 2024: Kutokana Jitihada Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kulinda afya za wananchi, wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilichopo Mlimani (UDSM) wamekuja na ubunifu wa kutengeneza gesi pamoja na vitambaa kwa kutumia mabaki ya chupa za plastiki jambo litakalosaidia na utunzaji wa mazingira pia.
Akizungumza leo, kwenye Maonesho ya 48, ya Kibiashara ya Kimataifa, yanayoendelea kufanyika Viwanja vya Sabasaba, jijini mwanafunzi kutoka katika hicho, Mbwelwa Felix amesema kuwa ameona waje na ubunifu huo ambao utasaidia kwenye utunzaji wa mazingira kwa kuondoka plastiki pamoja na kufaidika na bidhaa hizo.
“Tumekuja na miradi miwili ambayo inatokana na mabaki ya chupa za plastiki, ambayo tunachukua mabaki ya chupa za plastiki na kuchakata kisha tunazichemsha ndipo ule ujiuji wake tunatengeza kitu kama pamba ambapo zinatokea nyuzi ambazo ndiyo tunatengeza vitambaa kama hivyo unavyoviona, kuna vizito na vilaini, pia tunatengeneza kapeti zitokanazo na mabaki haya.
“Mradi wetu wa pili kwa kutumia mabaki haya tunayachakata na kuyaweka kwenye chemba na kuyeyusha hizi plastiki na kutengenezea mafuta ambayo yanapatikana kwenye hiyo chemba ambapo haturuhusu hewa kutoka wala kuingia ndani na kutengeneza gesi ya kupikia.
“Hii itasaidia kuifanya jamii kuacha kupikia nishati chafu ya mkaa na kuni na kusaidia utunzaji wa mazingira na kuwa salama kiafya.” Alimaliza kusema mwanafunzi huyo alipokuwa akitoa maelezo hayo kwenye banda lao.