The House of Favourite Newspapers

ARSENAL YAMTOKEA PACHA WA LACAZETTE

ARSENAL inaaminika imewasiliana na staa wa Olympique Lyon ya Ufaransa, Nabil Fekir kuhusu uwezekano wa kumsajili. Hata hivyo, dili hilo litategemeana kama wataweza kumuuza kiungo wao, Mesut Ozil.

 

Arsenal inataka kumsajili Nabil Fekir, ambaye katika siku nyuma aliwahi kutakiwa na timu za Ligi Kuu England. Fekir aliwahi kucheza na straika wa Arsenal, Alexandre Lacazette, ambapo walitengeneza kombinesheni ya kutisha kwenye safu ya ushambuliaji ya Lyon.

 

Lacazette, hata hivyo, alimwacha Fekir na kujiunga na Arsenal katika msimu wa 2017/18. Liverpool ilikaribia kumsajili mwaka jana wakati Tottenham Hotspur nayo imekuwa inatajwa kumtaka Fekir, ambaye pia anachezea timu ya taifa ya Ufaransa.

 

Kwa mujibu wa Gazeti la L’Equipe la Ufaransa ni kuwa, Arsenal imekuwa inahangaika kusaka timu ambayo inaweza kumchukua Mesut Ozil ili wapate fedha ya kusaka mbadala wake.

 

Ozil amekuwa analaumiwa kwa muda mrefu sasa kwa kushindwa kufanya vizuri na hasa kwenye mechi kubwa.

 

Arsenal inataka kumuuza Ozil baada ya kuona amekuwa mzigo katika klabu hiyo, ambayo inamlipa mshahara mkubwa wa kiasi cha pauni 350,000 (Sh. bilioni moja) kwa wiki. Katika msimu uliomalizika wa 2018/19, Ozil alijikuta mara nyingi akiwekwa benchi.

 

Hata hivyo, hakuna timu ambayo imeonyesha nia ya kumtaka kumsajili Ozil. Arsenal ipo sokoni ikisaka wachezaji ambapo kwa sasa imenasa straika wa miaka 18, Mbrazili Gabriel Martinelli.

 

Wachezaji wengine wanaohusishwa kutakiwa na Arsenal ni pamoja na beki wa kushoto wa Celtic, Kieran Tierney, 22 na beki wa St Etienne, William Saliba.

Comments are closed.