ASALI HAILAMBWI KWA NCHA YA KISU

ASALI Shoga wanakwambia raha ya mwanaume awe na madeni na mwanamke sharti alijue jiko siyo kukalia umbea hadi domo limekaa upande, upo nyonyo? Kama ulikuwa hujui jua sasa, hata kichungu nacho huonjwa ati, wareeeeereee!  Nashanga bia yenyewe moja lakini asubuhi na wewe unakimbilia mchemsho inahu? Paaaambeeee shoga, usione simba kaloa na mvua ukasema chui, fyaaaatuuuuu! Hili la leo sasa limeniganda kwenye koo, kutapika siwezi, kulimeza siwezi acha tu niwachambeee weee huenda likanitoka! Jitu zima linashindwa kuelewa kuwa hata paka mzee naye hutamani maziwa!

Siku zote nikisema kitu huwa namaanisha shoga yangu na usije kumtekenya hata siku moja aliyekubeba! Hivi hii tabia ya wanaume kutuchukulia sisi wanawake kama spea tairi bado ipo? Anakutongoza mnaelewana kila siku anaona raha ukimpa staili mpya akikuchoka anakubloku kila kona, shuuuutuuuu!

Kuna shoga yangu amenipa kisa cha ukweli, amenitoa machozi kama siyo kusisimka shoga yangu kisa bwana wake kumchezea kwa muda mrefu na mwisho wa siku kumuoa mtu mwingine na kuishia kuachwa kwenye mataa tena yale ya kwenye foleni Ubongo kama siyo Tazara. Anasema alikutana na bwana wake kwa mara ya kwanza ndani ya Mlimani City alienda kununua mahitaji si unajua tena kujiona Mzungu mara moja moja siyo kila siku kukimbilia gengeni kwa Juma Kisigono.

Basi shosti ile anaingia ndani, akichagua kitu jamaa yupo nyuma yake naye anachagua kama chake, wakati wa kupelekea kulipia hivyo vitu jamaa akachomoa pesa yake na kumlipia. Walipotoka nje ya hapo wakabadilishana namba za simu na huo ndiyo ukawa mwanzo wa uhusiano wao.

Shosti anakwambia, kweli mwanga siyo lazima atembee na ungo usiku, waliitana majina ya kila aina, viwanja alioneshwa hadi vingine ambavyo havijui! Si akaona hapo ndiyo pa kumpa mapenzi yote! Mwenzangu na mimi akajitoa kila walipokutana kosa ambalo hakulijua na analojuta hakuwahi kutambulishwa ukweni.

Jamaa baada ya kumtumia weeee, kumbe alikuwa ameshamchoka yaani kamuona kama bigijii imeshaisha utamu anataka kutafuta bigijii nyingine. Shosti mitandao yote akablokiwa, marafiki aliotambulishwa wote nao wakamkataa kama hawamjui vile. Siku ya siku, jiko likawekwa mkaa na kuwashwa! Taarifa za ndoa zikamfikia, kwenda kushuhudia kanisani hakuamini, akaenda hadi ukumbini roho ilimuumaje!

Nikugeukie sasa na wewe mwenzangu na mimi, kwanza nianze na mwanamke mwenzangu. Unakubali vipi kuchezewa kwa kipindi kirefu bila hata ukweni kukufahamu? Hata mawifi hawakujui bado unajiita una mchumba? Ni sawa na kulamba asali kwa ncha ya kisu jambo lisilowezekana.

Haya na wewe mwanaume, umeshaona mwenzako ni mwili wa majaribio, unauchezea unavyotaka mwisho wa siku ukamuoe mwingine inahu? Yaani ningekuwepo hiyo siku nahisi huyo aliyewafungisha ndoa mbona angejuuutaaa!

Mwanamke mwenzangu ifike wakati tubadilike, hayo ya kuchezeana na kupotezeana muda yalikuwa zamani siku hizi kila mtu mjanja! Ukiona ana dalili za kuchepuka angalia ustaarabu mwingine mapema, upo nyonyo? Kwa leo niishie hapa, tukutane tena wiki ijayo! Ni mimi Shangingi Mstaafu Anti Nasra.


Loading...

Toa comment