ASANTE! NGUVU YA KUMWAMBIA MPENZI WAKO NISAMEHE,

NI wiki nyingine tena Mungu ametukutanisha kupitia ukurasa huu. Naamini umzima na unaendelea na mchakamchaka wa maisha kama kawaida. Nikukumbushe tu kwamba, kuishi maisha mazuri unaamua wewe.

Kama utakuwa makini katika kila nyanja muhimu katika maisha yako, nakuhakikishia furaha itatawala katika maisha yako. Kumbuka tu kwamba, ili maisha yako yewe na furaha na amani pamoja na mambo mengine hakikisha uhusiano wako uko sawa.

Kama uko kwenye ndoa, mpende mwenza wako, mfanyie kila unaloona litamfurahisha na yeye atakufanyia pia. Mwisho wa siku kila mmoja achukue nafasi yake katika kutengeneza furaha ya mwezake.

Mpenzi msomaji wangu, kwenye hili la mahusiano leo nataka nikupe siri ambayo wengi hawaijui ya maneno ASANTE, SAMAHANI NA NAKUPENDA

Ni maneno ya kawaida sana ambayo huenda tunayasikia kila siku lakini nikuambie tu kwamba, kutamka maneno hayo kwa mpenzi wako, nguvu yake ni kubwa sana.

Ikumbukwe uliye naye anataka mara kwa mara kuhakikishiwa kwamba anapendwa, kwa maana hiyo kitendo cha wewe kila wakati kumwambia NAKUPENDA kinamfanya ajisikie amani ndani ya moyo wake. Ndiyo maana nakusihi sana usilipuuze neno hili pale inapobidi.

Lakini katika safari yenu ya maisha kuna kukoseana. Unaweza kusema ama kufanya jambo likamkwaza mpenzi wako. Katika hali hii kama kweli unampenda unachotakiwa kumwambia ni NISAMEHE MKE WANGU AU NISAMEHE MUME WANGU. Kwa kutamka maneno hayo wala huwezi kupungukiwa na chochote na badala yake utakuwa unaokoa penzi lako lisinyauke.

Kuwa mwepesi wa kuomba msamaha pale unapokosea kwani mbali na kwamba inaonesha utu lakini pia inadhihirisha kuwa huyo uliyenaye unampenda na huna dhamira ya kumkwaza. Tuache ubabe wa kutojali hisia za wenza wetu maana madhara yake ni makubwa ikiwemo penzi kufa.

Mbali na hayo, kuna hili neno ASANTE! Wakati mwingine unaweza kukuta mume anafanya jambo zuri kwa ajili ya mke wake lakini wala mke haoneshi kuthamini kwa kushukuru. Anaona kwa kuwa aliyemfanyia ni mume wake, ni wajibu wake hivyo haina haja ya kushukuru.

Kama wewe ni kati ya wanawake hao basi huijui nguvu ya kushukuru. Kumbuka kwamba hata kama ni mumeo lakini akikununulia zawadi, kusema asante inampa nguvu ya siku nyingine kukuletea. Kumbuka wapo ambao wako kwenye ndoa kama wewe lakini waume zao wala hawawafanyii wake zao mambo hayo.

Hata mnapokuwa kwenye uwanja wa mahaba, nazungumzia faragha. Kama mume amekupa raha uliyokuwa unaitaka, kusema ASANTE MUME WANGU kwa penzi nono, kunanogesha penzi na kutamfanya kila wakati akufurahishe. Kwani ukitamka hivyo unapungukiwa nini? Anza leo tabia ya kushukuru, hiyo itakuwa sehemu ya mbolea ya kulistawisha penzi lako.

Nihitimishe kwa kusema kwamba, kuna mambo madogo madogo ambayo baadhi ya watu walio kwenye mahusiano wanayapuuza lakini nguvu yake ni kubwa katika kuboresha penzi. Mimi nakushauri anza kwa kuyatamka maneno hayo hapo juu pale inapobidi.

Tukutane tena wiki ijayo.


Loading...

Toa comment