The House of Favourite Newspapers

ads

Baada ya Mwanaye Kuwa Staa, Baba Zuchu Aibuka!

0

BAADA ya mwanaye kuwa staa mkubwa Bongo, hatimaye baba mzazi wa mwanamuziki ambaye kwa sasa ndiye first lady wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Zuhura Othman Soud ‘Zuchu’, Othman Soud ameibuka. Baba huyo wa Zuchu amefunguka mambo mazito, baada ya kuwepo kwa maneno mengi, huku wengi wakiwa hawamjui.

 

NI BABA HALALI…

Othman amesema kuwa, yeye ndiye baba mzazi wa Zuchu na ataendelea kuwa baba wa mwanamuziki huyo.

TUJIUNGE ZANZIBAR

Akizungumza na www.globalpublishers.co.tz katika mahojiano maalum (exclusive interview), baba huyo ambaye makazi yake ni visiwani Zanzibar, ameweka wazi mambo ambayo baadhi ya watu walikuwa hawayafahamu juu ya Zuchu ambaye ni staa mpya wa Bongo Fleva;

 

IJUMAA WIKIENDA:

Baba shikamoo…

OTHMAN: Marahaba, karibu ninakusikiliza…

IJUMAA WIKIENDA: Kwanza hongera sana kwa mtoto wako ambaye amekuwa akijitahidi sana kwenye muziki na sasa hivi jina lake linasikika kila kona.

OTHMAN: Asante sana, Mungu ni mwema, amemuinua mwanangu na mimi naendelea kumuombea siku zote.

IJUMAA WIKIENDA: Ninakumbuka na wewe ulikuwa muimbaji mzuri wa Taarab enzi za Kundi la Muungano, je, hadi sasa bado unaendelea kuimba?

OTHMAN: Hapana, mimi nilishaachana na muziki kitambo na nikajiunga na jeshi Unguja na sasa hivi nimestaafu, naendelea na biashara zangu tu.

IJUMAA WIKIENDA: Zuchu amekuwa akifanya matamasha mbalimbali makubwa kama lililofanyika miezi michache iliyopita kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar, lakini hukuonekana halafu kuna madai ya mitandaoni kwamba, ulimtelekeza. Je, hii imekaaje?

OTHMAN: Mimi sina taarifa yoyote, hivyo mimi ni mtu mzima, siwezi kutoka huku niende bila taarifa, nitakuwa ninajishushia heshima pia, na kuhusu kumtelekeza hiyo siyo kweli na hata Bi Khadija hawezi kusema hivyo.

IJUMAA WIKIENDA: Kwani yeye Zuchu hajawahi kukuambia au kukupa mualiko? OTHMAN: Hapana, hajawahi kuniambia chochote kile.

IJUMAA WIKIENDA: Lakini si mnawasiliana kwa simu?

OTHMAN: Hapana, hatuna mawasiliano kwa sasa, nakumbuka mara ya mwisho nilizungumza naye alikuwa akiuza duka maeneo ya Kinondoni-Studio (Dar), hadi leo sijawasiliana naye, ni siku nyingi zimepita kwa kweli sijaongea naye wala kumuona.

IJUMAA WIKIENDA: Kwani kuna tatizo kati yako na yeye au mama yake, Bi Khadija?

OTHMAN: Unajua kwenye maisha, unaweza kuonekana wewe ni mtu ambaye hufai, lakini ukweli nitabaki nao mimi na sipendi kumfaidisha mtu kwa sababu yeye Bi Khadija hakuwa na uhusiano wa karibu na baba yake kabisa, lakini alipoingia TOT alimtafuta baba yake, wakawa vizuri na amemlea mpaka Mungu alipochukua uhai wake hivi karibuni. Sasa mbona yeye hakumtenga baba yake hadi afanye hivyo kwa mwanaye (Zuchu)?

IJUMAA WIKIENDA: Sasa kwa nini usiamue tu kuchukua jukumu la kumtafuta yeye (Zuchu), wewe kama baba?

OTHMAN: Unajua unaweza kufanya hivyo, lakini ukaonekana kama unajipendekeza kwa sababu labda sasa hivi Zuchu anaimba au amekuwa maarufu, lakini huko mimi sipo.

IJUMAA WIKIENDA: Kama sasa hivi Zuchu akija nyumbani Zanzibar muyaweke sawa, inakuwaje? OTHMAN: Mimi sina shida kabisa, yule ni mwanangu na mimi ni baba yake na haiwezi kubadilika kabisa hiyo na mimi namuombea kwa Mungu siku zote.

IJUMAA WIKIENDA: Haya baba nakushukuru sana kwa ushirikiano wako. OTHMAN: Haya asante sana, karibu tena.

MZEE CHENGA ALINENA HAYA…

Hivi karibuni, aliyekuwa Mkurugenzi wa Kundi la Taarab la Muungano ambalo Khadija na Othman walikuwa waimbaji wake, Nobert Chenga alikiri kuifahamu familia hiyo na kwamba wakati Zuchu anazaliwa, wawili hao walikuwa kwenye kundi lake hilo.

Mzee Chenga alikwenda mbele zaidi na kusema kuwa, wakati familia ya Othman na Bi Khadija inahamia Bara (Dar), yeye ndiye alikuwa mwenyeji wao.

ZUCHU NA WCB

Zuchu amesajiliwa kwenye lebo hiyo kubwa na kufanikiwa kupata mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi, ambapo nyimbo zake zimefanya vizuri sana huko mjini YouTube ikiwemo Raha na Cheche!

STORI: IMELDA MTEMA, DAR

Leave A Reply