The House of Favourite Newspapers

Baba Kichuya Afikishwa Polisi – Video

BAADA ya kudaiwa kunyweshwa sumu kisha kutekwa na kuporwa gari na baadaye kutupwa kwenye mashamba ya Chuo cha SUA mjini hapa, dereva maarufu wa teksi, Ramadhan Kichuya ambaye ni baba mzazi wa winga wa Simba Sc na Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Shiza Kichuya amefikishwa Polisi na mmiliki wa gari aliloporwa aina ya Toyota IST.

 

Wakati hayo yakijiri, mwanaye huyo, Shiza amekuwa akilaumiwa na wananchi kwa kushindwa kufika kumjulia hali baba yake na kumsaidia kwenye tukio hilo baya.

Baadhi ya wananchi wa ndani na nje ya Mkoa wa Morogoro waliofuatilia tukio hilo lililoripotiwa na gazeti ndugu la hili, Amani na Global TV wiki iliyopita, wameeleza kuguswa na tukio hilo la kusikitisha.

“Inasikitisha maana, pamoja na kulishwa sumu, kuteswa na kutupwa porini, mwenye gari amesubiri tu baba Kichuya ametoka hospitalini, naye amemtia ndani.

 

“Kiukweli kama watu wanavyosema mwanaye Shiza angemsaidia kwani awali nilipomuona baba Kichuya na hilo gari jipya kabisa, nilijua mwanaye amemnunulia,” alisema Selemani Chande, mkazi wa mjini hapa.

Baada ya kusikia malalamiko hayo ya wananchi, Ijumaa Wikienda liliingia mzigoni ambapo lilifanikiwa kuzungumza na baba Kichuya ambaye alithibitisha kupelekwa Polisi, sambamba na mwanaye huyo kutofika tangu akumbwe na mkasa huo wa kusikitisha.

 

“Ninamshukuru Mungu ninaendelea vizuri. Pia nakushukuru wewe (mwandishi) ulikuwa unakuja hadi wodini kunijulia hali na kuripoti tukio hili.

“Ni kweli baada ya kutoka tu hospitalini, tajiri ambaye ni mmiliki wa gari nililoporwa alinipeleka Polisi ambapo walichukua maelezo yangu na kuniruhusu kurejea nyumbani.

 

“Walidai watakaponihitaji wataniita.

“Pia ni kweli mwanangu Shiza tangu nikumbwe na matatizo haya hajaja kuniona ila mara kwa mara ananipigia simu na kunijulia hali. Sina kinyongo naye kwa kuwa ana majukumu ya mechi za kimataifa na timu yake ya Simba na pia Timu ya Taifa,” alisema baba Kuchuya.

 

Awali, wakati baba yake akiwa hoi wodi namba 9 ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, mwandishi wetu alimpigia simu Shiza aliyedai taarifa za baba yake kudaiwa kulishwa sumu kisha kuporwa gari anazo na kwamba yuko njiani kwenda kumuona.

STORI: DUNSTAN SHEKIDELE, MOROGORO

 

BABA KICHUYA ATEKWA! Anyweshwa Sumu!

Comments are closed.