Balinya atoa ahadi ya mabao Yanga

STRAIKA wa Yanga, raia wa Uganda, Juma Balinya, amewaambia mashabiki wa timu hiyo ataanza kutupia kwenye mechi ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakayocheza na Township Rollers baada ya kushindwa kufanya hivyo katika mchezo wao uliopita wa kirafiki mbele ya Kariobangi Sharks.

Balinya aliyefunga mabao 19 akiwa na Polisi ya Uganda msimu uliopita, Jumamosi hii ataiongoza safu ya ushambuliaji ya Yanga kupambana na Rollers ya Botswana katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo itapigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Straika huyo amesema kuwa mashabiki wa Yanga wataanza kufurahia mabao yake wakati ambao atapambana na Rollers katika mechi hiyo ya kimataifa baada ya kutofanikiwa kufunga bao lolote mbele ya Sharks na mwisho mechi hiyo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

 

Bao la Yanga katika mechi hiyo lilifungwa na Patrick Sibomana kwa njia ya
penalti. “Kwanza niwashukuru mashabiki wote wa Yanga kwa kile ambacho walitufanyia katika Wiki ya Mwananchi. Walikuja kwa wingi kwa ajili ya kutusapoti jambo ambalo lilitufanya tujisikie vizuri.

 

“Lakini kwa matokeo ya mechi ile haikuwa jambo baya ambalo tulifanya kwa sababu ndiyo mechi yetu ya kwanza kubwa, lakini pia niwaambie kwamba ni suala la muda pekee kabla ya kuona mambo mazuri. Tuna kikosi kizuri hadi sasa, ninawaahidi mtafurahi katika msimu ujao wa ligi pamoja na ligi ya mabingwa katika mchezo wetu huu na Rollers,” alisema Balinya.


Loading...

Toa comment